WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) umekutana na wadau mbalimbali kutoka serikalini na sekta binafsi kwa lengo la kukusanya maoni yao kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Utoaji Leseni za Biashara ya mwaka 1972.
Akizungumza Mkurugenzi wa Leseni wa Brela, Andrew Mkapa alisema hatua hiyo pamoja na mambo mengine imelenga kuongeza wigo kwa kuweka mazingira mazuri ya biashara nchini.
Alisema mchakato wa kubadilisha sheria hiyo sura 208 ya mwaka 1972, ulianza kwa uundaji wa kikosi kazi maalumu kilichokuwa na jukumu la kuipitia sheria hiyo kulingana na hitaji. Alisema sasa umefika muda wa kupata maoni ya wadau kabla ya hatua zingine za kuiletea mabadiliko.
“Mchakato wa marekebisho wa sheria hii umekuwa ukifanyika kwa nyakati tofauti kulingana na mahitaji, hadi leo tunapokutana kuijadili tayari sheria hiyo imeshafanyiwa marekebisho mara 30, hivyo ni muhimu kupata maoni yenu kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya ufanyaji wa biashara,” alisema.
“Kuna mahitaji katika ufanyaji biashara ambayo kutokana na uwapo wa sheria hiyo, kunahitajika marekebisho kwa ajili ya kuongeza ufanisi, hivyo tukiwa kama wahusika wakuu katika hilo tumeona ni busara kukutana na wadau ili kupata mawazo yenu,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Mkapa, kikao hicho cha wadau kitasaidia kuleta mwelekeo mpya katika utoaji wa leseni kwa ajili ya kuboresha huduma kwa wananchi na nchi kwa ujumla katika kipindi hiki ambacho mazingira ya biashara yanazidi kukua.