SERIKALI imewaalika mashirika binafsi ikiwemo watoa huduma wa mawasiliano na wadau mbalimbali wa maendeleo kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa mfumo wa m-mama hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye bungeni leo Agosti 29, 2023 alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Santiel Kirumba.
Mbunge huyo alihoji serikali haioni haja ya kuhimiza mashirika mengine ya simu kujiunga na Mpango wa m-mama, kwani umekuwa msaada kwa wajawazito wengi.
“Mfumo wa m-mama unatekelezwa na kusimamiwa na Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya vodacom, USAID, Vodafone Foundation, Pathfinder International na Touch Foundation.
“Mfumo huu unalenga kusaidia upatikanaji wa usafiri wa dharura kwa mama mjamzito, mama aliyejifungua na mtoto mchanga kote nchini.
“Mheshimiwa Spika, ili kufikia malengo ya Mfumo kwa haraka na kufikia walengwa wengi zaidi, kuna haja ya wadau mbalimbali kuongeza nguvu kwa kushirikiana katika utekelezaji wakiwemo watoa huduma wengine wa mawasiliano.
“Hivyo, natumia fursa hii kuwaalika mashirika binafsi wakiwemo watoa huduma wengine wa mawasiliano pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo wajitokeze kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa Mfumo wa m-mama hapa nchini,” amesema Waziri Nape.
–
Comments are closed.