Wadhibiti Madini yaliyokuwa yakitoroshwa

MBEYA: MADINI yenye thamani ya Sh milioni 961 yenye uzito wa kilogramu 6.93 yamekamatwa Wilaya ya Chunya , mkoani Mbeya yakitoroshwa kwenda kuuzwa nje ya nchi.

Hayo yamebainishwa leo Oktoba 28, 2023 na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde katika ziara ya kikazi mkoani Mbeya katika machimbo ya dhahabu wilayani Chunya.

Mavunde amesema dhahabu iliyokamatwa ina thamani ya zaidi Sh milioni 961 ambapo kama ingetoroshwa Serikali ingekosa mapato ya zaidi Sh milioni 68.

Akizungumza na wafanyabiashara wa Madini katika soko la madini Mbeya Mavunde amewataka wafanyabiara wote wa madini kutojihusisha na njama zozote za utoroshaji madini kwani kufanya hivyo kunakosesha mapato ya nchini na kudumaza juhudi za kuleta maendeleo.

“Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira ya dhati ya kuikuza sekta hii ya madini,hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunafanya biashara hii kwa uadilifu,uaminifu na uzalendo mkubwa”, Amesema Mavunde na kuongeza.

” Wafanyabiashara wa madini nawatangazia tena kuacha kujihusisha na utotoshaji wa madini,tutachukua hatua kali kwa watu wote wanaohusika bila kusita.” Amesema.

Aidha, ameushukuru uongozi wa Mkoa wa Mbeya chini ya Mkuu wa Mkoa Juma Homera kwa ushirkiano mkubwa wanaotoa kudhibiti utoroshaji.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mayeka Mayeka amesema kuwa mazingira ya uchimbaji madini wilayani Chunya yanaendelea kuhimarishwa isipokuwa changamoto kubwa ni utoroshaji madini na wizi wa carbon katika mialo ya uchenjuaji.

 

Habari Zifananazo

Back to top button