Waeleza changamoto waajiri wapya vituo vya kazi

WAKURUGENZI mbalimbali  kutoka sekta binafsi nchini  wamesema baadhi ya wahitimu wana changamoto  ya jinsi ya kuwasiliana na waajiri wanapopata kazi.

Hayo yamebainika katika mjadala ulioandaliwa kwa wakurugenzi mbalimbali kutoka sekta mbalimbali za kifedha, kilimo, teknolojia, uzalishaji na viwanda na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ( UDSM) kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET).

Akizungumza katika mjadala huo, Mkurugenzi kutoka Multi Choice, Jacqueline Woiso ameeleza uwezo wa wahitimu hao katika kufanya kazi ni changamoto kubwa ya muda mrefu hivyo UDSM iangalie vitu vya kuongeza katika mitaala yao kuwawezesha wanafunzi  kuwa bora katika mawasiliano.

“Kuangalia wanafunzi wanawasiliana vipi na mabosi wao, wenzao wanaofanya nao kazi, wateja wa taasisi na wengineo,” amesema.

Ametaja changamoto nyingine kwa wahitimu hao ni uwezo wa kutoa huduma kwa wateja.

“Wahitimu wengi wakiajiriwa bado tunapata shida kumuelimisha mteja ni mfalme ambaye anapaswa kuhudumiwa vizuri,” amesema.

Ameongeza pia kwenye eneo la maadili wahitimu hao wamekuwa na changamoto kubwa katika kazi, kwani hukaa muda mfupi kazini na hapo hapo hutaka kuwa na pesa nyingi mwisho wa siku wanaanza wizi kwa njia mbalimbali.

Jambo lingine anaeleza wahitimu hao hawana fikra za kibiashara kwani wanapaswa kuelewa kuwa ili utengeneze hela juhudi binafsi inahitajika.

Naye Mgeni Rasmi katika mjadala huo alikuwa Waziri wa Nchi kutoka Ofisi ya Rais Zanzibar, Jamal Kassim Ali ambaye amesema UDSM na sekta binafsi wanajadiliana kuona namna nzuri ya kuweza kuwasaidia wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu waweze kuajirika ama kujiajiri.

“Kukutana huku ni kuangalia UDSM ambayo inazalisha wahitimu wengi ni namna gani waweze kuajirika ama kujiajiri pindi wanapomaliza,” amesema.

Amesema kupitia mradi wa HEET serikali imefanya jitihada ya kutafuta fedha kwa lengo la kuboresha mitaala itakayofundisha vijana ambayo itaendana na mahitaji ya soko.

Kwa upande Wake Makamu Mkuu wa  UDSM , Profesa William Anangisye amesema wamekutana kwa ajili ya mazungumzo ya kimkakati kati ya chuo hicho na wadau kutoka sekta binafsi.

Amesema lengo ni kuhakikisha wanatekeleza mradi wa HEET ili kuweze kuwa na mafanikio katika hayo mageuzi ya elimu.

“Ni lazima tuwe na wahitimu ambao uwezo wao na mtazamo ni kusaidia nchi kuleta mageuzi,” amesema. Amesema lengo la UDSM ni kujifunza kwa wadau ambao wako kwenye sekta binafsi.

“Huu ni mkakati tumekutana na wakuu wa taasisi wao watasaidia kutueleza changamoto wanazokutana nazo kupitia wahitimu wetu,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania ( TPSF), Raphael Maganga amesema wao kama sekta binafsi wamegundua kuna changamoto kubwa kwa wahitimu wanaomaliza vyuo vikuu.

Amesema hivyo wanaangalia ni jinsi gani wapo tayari wa kuwapatia ujuzi ili kuwe na ushindani. “Ukiwa na elimu ni kitu kimoja na ujuzi ni kitu kingine,” amesema.

Amesema kumpatia mtoto ujuzi sio suala la serikali au sekta binafsi bali na wazazi wanahusika hivyo wawaruhusu watoto wao kufanya kazi wakiwa vyuoni.

Habari Zifananazo

Back to top button