Waeleza teknolojia ya kuchuja maji mabwawa ya samaki
“Mara nyingi samaki wakiwa na uchafu kwenye bwawa wanakufa.
“UDSM tumekuja na mfumo ambao unachuja yale maji ili wale samaki wapate kuishi na kuwekwa samaki wengi zaidi kwenye bwawa,” hiyo ni kauli ya Mhitimu wa Sayansi ya Bahari na Teknolojia ya Uvuvi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Joshua Atata.
Atata amesema hayo katika maonesho ya Nanenane kitaifa yanayoendelea mkoani Mbeya.
Amesema teknolojia hiyo ipo kwenye mfumo wa kutumia maji machafu kuyachuja ili yaweze kuendelea kutumika tena.
Ameeleza mfumo huo una sehemu kuu nne ya kuchuja kwa kuwa wanatumia kokoto ambazo zinaondoa uchafu mkubwa kwenye maji.
Lakini pia amesema wanatumia chaza ambao ni jamii ya konokono kwa ajili ya kula viumbe wadogo walioko kwenye maji ambao wanasababishwa na uchafu unaokuwepo kwenye maji.
“Pia kuna maganda ya nazi ambayo ni mepesi sana yamewekwa kwa ajili ya kukuza bakteria ambao wanasaidia kutengeneza mbolea kutokana na uchafu wa samaki.
“Sehemu ya nne kuna mimea inaitwa azola au magugu maji hiyo mimea inategemea sana mbolea iliyotoka kwa samaki kwa hiyo mbolea iliyotoka kwenye mfumo mzima inatumiwa na hiyo mimea ambayo inaitwa magugu maji kuondoa uchafu uliozalishwa na samaki,” amesema.
Amesema baada ya hatua zote hizo mfumo unarudi na maji yanakuwa masafi hapo tayari viumbe wengine wamekuwa wamevunwa.
“Kiufupi huu mfumo ni kwa ajili ya kuchuja maji kwa ajili ya ufugaji wa samaki na kupitia mfumo huu samaki wanazalishwa mara mbili zaidi ya mfumo wa kawaida,”amesema.
Ameeleza lengo kubwa la teknolojia hiyo ni kuongeza uwezo wa mkulima kuwa na idadi kubwa ya samaki kwenye bwawa dogo lakini kwa wakati huo huo ana uwezo wa kuvuna zaidi ya kitu kimoja kwenye mfumo mmoja.
Amesema hapo atavuna samaki, chaza ambao wanauzika na pia ni mapambo, lakini atavuna jamii ya magugu maji ambayo ni chakula cha kuku na chakula cha ng’ombe lakini ni chakula cha nguruwe.
Naye Ofisa Uhusiano chuoni hapo katika Kitengo cha Mawasiliano na Masoko, Zamda George amesema mbali na kuonesha teknolojia za kilimo pia uwepo wao katika maonesho hayo ni kufanya udahili.
“Tumekuja na ndaki ya kilimo na teknolojia ya chakula na shule kuu ya sayansi ya akua na teknolojia ya uvuvi,” amesema.