Waendesha Baiskeli 100 kushindana Arusha
ARUSHA: Waendesha Baiskeli 100 watachuana vikali katika mbio za mchezo huo ambazo zimepangwa kufanyika Oktoba Mosi jijini Arusha.
Mashindano hayo yanajulikana kama ‘Tanzania Heritage tour ‘ yameandaliwa na kampuni ya Tanzania Cycling kushirikiana na chama cha mchezo wa baiskeli Mkoa wa Arusha (ACA)
Joel Senny, Mkurugenzi wa kampuni ya Tanzania cycling amesema mashindano hayo yatajumuisha waendesha baiskeli wanaume ,wanawake na wazee ambao watashindana kwa umbali tofauti.
Amesema katika kundi la wanaume watashindana kilometa 150, wanawake wataendesha kwa kilometa 100 huku washiriki wenye umri wa miaka 47 na zaidi watahusika katika umbali wa kilometa 100.
“Mashindano ya baiskeli yanaweza kutumika kuelimisha jamii kwa mambo mbalimbali ya kimaadili pia kuhamasisha utalii wa michezo na kwa tukio hili tutakuwa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa mkoani Arusha (TAKUKURU) ambao watashiriki nasi.”amesema Senny.
Florence Mwita, Mkuu wa dawati la elimu kwa umma kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoani Arusha amesema watashiriki katika mbio hizo na watatumia tukio hilo kutoa elimu kuhusu mapambano dhidi ya Rushwa.
“Tutatumia nafasi hiyo kuelimisha na kukutana na jamii kutoa elimu na kwa sababu tuna nia ya kuhakikisha shughuli za jamii zinafanikiwa tutachangia moja ya zawadi za washindi ili kuunga mkono tukio hilo la michezo,”amesema Mwita.