Wafanya maadhimisho jaribio kuipindua serikali

LEO Waturuki waliopo hapa nchini wameungana na Waturuki wenzao pote duniani kufanya maadhimisho ya saba ya ushindi dhidi ya jaribio la kuipindua Serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan mwaka 2016.

Tukio hilo lililotokea Julai 14 mwaka 2016 liligharimu maisha ya watu 251 na kujeruhi wengine 2,196.

Advertisement

Hayo yamebainishwa na Balozi wa Uturuki nchini, Dk Mehmet Gulluoglu kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.

Katika programu iliyoandaliwa na ubalozi wake jana ya kuwakumbuka wananchi hao waliuawa katika tukio hilo la Julai 14, Balozi Gulluoglu alisema Julai 15 kila mwaka ni siku inayokumbukwa kwa kushinda jaribio hilo la kimapinduzi dhidi ya serikali yao.

Alisem tukio liliandaliwa na kundi moja linalodaiwa kuwa la kigaidi nchini humo kwa lengo la kutaka kumuua Rais Erdogan na kulipua jengo kuu la Bunge nchini humo.

Akizungumzia tukio hilo katika maadhimisho ya mwaka jana, Dk Gulluoglu alisema ushindi huo ni wa wananchi wote wa Uturuki waliosimama kidete kupinga mapinduzi hayo.

Alisema tangu hapo, Julai 15 kila mwaka inajulikana kama ‘Siku ya Demokrasia na Umoja wa Kitaifa’ kutokana na wananchi kujitokeza kwa wingi kupinga jaribio hilo la kuipindua serikali.

“Wananchi walizima jaribio hilo la mapinduzi, walizuia vifaru vya waasi kwa mikono yao, wakati jaribio hili la kuipindua serikali likitokea, nilishuhudia kwa macho nikiwa Mji Mkuu Ankara,” alisema wakati huo Dk Gulluoglu.

Alisema maeneo mbalimbali yalishambuliwa likiwemo Bunge la nchi hiyo na jengo la polisi huku wananchi wakiweka upinzani mkali dhidi ya waasi hao.

Aidha, vyombo mbalimbali vya habari wakati huo viliripoti kuwa baada ya taarifa za serikali ya Rais Erdogan kutaka kupinduliwa, maelfu ya wananchi wa Uturuki waliingia mitaani licha ya mashambulizi kutoka kwa waasi hao na baada ya muda saa chache walifanikiwa kuzima jaribio hilo.

Kutokana na ushindi huo, Serikali ya Uturuki iliamua kutenga Julai 15 kila mwaka kama siku ya ‘Demokrasia na Umoja wa Kitaifa.’

1 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *