Wafanya upasuaji wa kwanza kwa Mama mjamzito

SONGWE: HOSPITALI ya Wilaya ya Songwe katika Mkoa wa Songwe imefanikiwa kufanya upasuaji wa kwanza kwa mama mjamzito baada ya kukamilika kwa hospitali hiyo hivi karibuni.
Hospitali hiyo inatajwa kuwa suluhu kwa wakazi wengi wa Songwe hasa akina mama na watoto waliokuwa wanasafiri umbali wa zaidi ya kilomita 80 kufuata matibabu.
Upasuaji huo umefanyika Oktoba 10, 2023 ikiwa zimepita siku nane tangu hospitali hiyo ilipoanza kutoa huduma za mama na mtoto, kulaza wajawazito na upasuaji kwa wajawazito ambapo huduma zingine za matibabu kwa wagonjwa wa nje (OPD) zilianza kutolewa Juni, 2020 na zinaendelea kutolewa.

Akizungumza akiwa katika hospitali hiyo baada ya upasuaji huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dk Ntufye Kapesa amesema kuwa upasuaji huo wa kwanza umefanyika jana Jumanne Oktoba 10, 2023 ambapo mama na mtoto wa kiume wapo salama.
Dk Kapesa amesema kuwa huo ni upasuaji wa kwanza tangu hospitali hiyo ianze kupokea wajawazito kwaajili ya kujifungua tangu Oktoba 2 mwaka huu, ambapo tayari wajawazito wengine 17 wameshajifungua kwa njia ya kawaida.

Kwa upande wake mama aliyefanyiwa upasuaji huo, Dotto Kwimba amesema anawashukuru madaktari hao kwa huduma nzuri waliyompatia.
Hivi karibuni Waziri wa Afya Ummy Mwalimu alipofanya ziara mkoani Songwe aliwaahidi Wananchi wa Wilaya ya hiyo kuwa hospitali hiyo itaanza mara moja kutoa huduma hizo,baada ya kusikiliza kilio cha Wananchi hao kuhusu adha wanayopata wakati wa kujifungua hasa pindi wanapohitaji kufanyiwa upasuaji.



