WIZARA ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imewaita wafanyabiashara katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), barani Afrika na kwingineko duniani, kutumia fursa ya mazingira mazuri ya biashara yaliyowekwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuja kuwekeza Tanzania.
Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alibainisha hayo mwanzoni mwa wiki wakati akizungumza na HabariLEO Afrika Mashariki kuhusu Maonesho ya 22 ya Biashara ya Wafanyabiashara Ndogo na za Kati ya EAC maarufu, Juakali/ Nguvukazi, yaliyofanyika Kampala Uganda Desemba 8 hadi 18, mwaka huu.
Maonesho hayo yaliwahusisha washiriki zaidi ya 1,500 kutoka nchi za EAC za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Uganda huku Tanzania ikiwakilishwa na wajasiriamali 300 na vijana 16 waliomaliza masomo ya vyuo wanaojifunza biashara ya mipakani mwa nchi.
Alisema Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia, imeweka vivutio vingi na mazingira rafiki na wezeshi kwa biashara na uwekezaji hivyo, Watanzania na watu wa EAC wajitokeze kufanya biashara na uwekezaji nchini.
“Mazingira ya biashara na uwekezaji kwa sasa ni mazuri sana kuliko ulivyokuwa nyuma maana kero nyingi za kibiashara zimetatuliwa na kubwa zaidi, wafanyabiashara wadogo, wa kati na hata wakubwa nchini wazingatie ubora ili kukabili ushindani katika soko la EAC,” alisema Kigahe.
Kwa mujibu wa naibu waziri huyo, Rais Samia amekwishaagiza wafanyabiashara wadogo, wa kati na sekta binafsi kwa jumla kusaidiwa ili kuzalisha zaidi na kuongeza tija.
Alisema uwekezaji mkubwa unahitajika nchini katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya kuongeza thamani ya mazao ili kuuza bidhaa, badala ya kuuza malighafi kwa bei ya chini kisha kununua bidhaa zilizotokana na malighafi hizo kwa bei ya juu.
“Tunahitaji zaidi kufanya ujasiriamali wa kutafuta masoko kwa ajili ya bidhaa tunazozalisha maana kuzalisha bidhaa ni hatuamoja, na kutangaza bidhaa kisha kuingia sokoni, ni hatua nyingine,” alisema.
Akaongeza: “Waje wawekeze na kuongeza thamani za mazao na rasilimali ili badala ya kuuza mahindi, tuuze unga na vyakula vya mifugo; tutangaze na kupata soko…”
Kwa mujibu wa Kigahe, Watanzania wanapokwenda katika maonesho mbalimbali ya kibiashara yakiwamo ya Juakali yanayotarajiwa kufanyika nchini Burundi mwaka kesho, wayatumie kutangaza fursa lukuki za kiuchumi zilizopo nchini ili kuvutia uwekezaji.
“Aidha, wajifunze mambo na mbinu mbalimbali za uzalishaji na biashara kutoka kwa wenzao wa nchi nyingine,” alisema na kuongeza: “Tutumie maendeleo ya miundombinu ya biashara kwa kuuzia bidhaa katika maeneo maalumu kama wanavyofanya wenzetu, na tuachane na kasumba ya kuuzia vitu barabarani na vichochoroni.”
Comments are closed.