KATAVI; Asilimia 55 ya wafanyabiashara 12,000 waliosajiliwa mkoani Katavi wamebainika kushindwa kutoa risiti za kielektroniki wafanyapo mauzo, hali inayoelezwa IMEsababishwa na ukosefu wa elimu ya mlipakodi.
Hayo yamebainika katika kampeni ya mlango kwa mlango inayofanywa na Mamlaka ya Mapatao Tanzania (TRA) Mkoa wa Katavi, yenye lengo la kutoa elimu kwa mlipakodi.
Meneja wa TRA Mkoa wa Katavi, Nicholaus Migera, amesema dhumuni la kampeni hiyo ni kutoa elimu mlango kwa mlango kwa mkoa mzima, ili kuwapa ufahamu walipa kodi wote na kujua changamoto zao, kuzitathmini, kuzichambua na kuona namna ya kuzitatua.
Amesema utoaji wa risiti za kielektroniki hauridhishi kwa mujibu wa taarifa ya mwezi Machi mwaka huu, ambapo amesema asilimia 45 ya wafanyabiashara ndio wenye uwezo wa kutoa risiti za kielektroniki.
Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara mkoani Katavi, wameiomba TRA kuwa na utaratibu wa kutoa elimu ya mlipakodi mara kwa mara kutokana na ongezeko la wafanyabiashara wapya.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amewataka TRA Katavi kutatua changamoto zote zilizowasilishwa kupitia Mwenyekiti wa wafanyabiashara, huku akiwataka kulipia kodi pasipo kushurutishwa.
Pia amewataka wafanyabiashara kuitumia vizuri elimu watakayopatiwa, kwani kulipa kodi ni moja ya kuichangia Serikali katika ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya maendeleo.