Wafanyabiashara Misenyi waonywa kanuni za afya

Wafanyabiashara Misenyi waonywa kanuni za afya

IDARA ya afya Halmashauri ya Misenyi na Kata ya Mutukula mkoani Kagera, imetangaza  kuwafungia wafanyabiashara wote,  ambao hawafuati afua za afya, ikiwa ni kuweka maji,  sabuni, pamoja na vitakasa mikono kwenye biashara zao.

Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi,  Dk Daniel Chochole, ametangaza uamuzi huo leo Septemba 8,2022,  baada ya  Kaimu Mkurugenzi  Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma  Dk Ama Kasangala kutembelea katika kata ya Mutukula kama sehemu ya kushirikisha jamii katika utoaji wa elimu  kukabiliana na Ebola.

Dkt Chochole amesema kwa kushirikiana na viongozi wa mitaa, wameweka utaratibu kila mfanyabiashara eneo la Mutukula, Misenyi na maeneo mengine ya Mkoa wa Kagera kuweka ndoo, maji tiririka pamoja na sabuni, ili kudhibiti  mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.

Advertisement

“Tumekuta kuna baadhi wameweka ndoo, lakini kuna baadhi hawajaweka zile ndoo za maji kwa ajili ya kunawa kama uongozi wa wilaya kupitia idara ya afya  kwa kushirikiana na  viongozi wa kata hii ya Mutukula na Misenyi tunatoa agizo kwa mfanyabiashara yeyote atakayekaidi agizo hili hadi Jumatatu mfanyabiashara yeyote ambae hatoweka vifaa vya kujikinga na Ebola  atafungiwa kufanya biashara yake,” amesesma Chochole na kuongeza

“Ni heri tubaki na wafanyabiashara wachache ambao watatusaidia ugonjwa kutoingia, kuliko kuwa na wafanyabiashara ambao watatuletea majanga,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Elimu ya Afya Dk Ama Kasangala, akipita maeneo mbalimbali ya Mutukula kutoa elimū ya viashiria vya ugonjwa wa Ebola na namna ya kujikinga.

Naye Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Dk Ama Kasangala, amesema wameendelea kurudi maeneo hayo kwa sababu ni mpakani na jitihada  za kwanza wanazofanya ni kushirikisha zaidi viongozi wa maeneo husika, kwani wao ndio wanaokaa karibu zaidi na wananchi.

“Tumejikita zaidi kushirikisha jamii kutoa elimu na kuhamasisha wananchi, na viongozi wa maeneo husika,  kwani wao ni sauti ya wananchi katika mtaa  hii  inasaidia kuhamasisha na tunarudi mara kwa mara maeneo haya kwa sababu ni mpakani,” amesema Ama na kuongeza:

“Mpaka ni eneo tu linalotutenganisha, lakini wanadamu tunaingiliana,  mfano hapa Mutukula hauwezi kutambua huyu Mtanzania au huyu Mganda, ugonjwa hauna mpaka,”amesema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *