Wafanyabiashara wa mazao nje ya nchi,watakiwa kurasimisha biashara zao.
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) imeanza kutekeleza maagizo ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk, Ashatu Kijaji kwa kukutana na wafanyabiashara wa mazao nje ya nchi, Mkoani Arusha na kurasimisha biashara zao ili zitambulike na wafanye kazi ya usafirishaji nje ya nchi .
Akizungumza Jijini Arusha wakati akifungua mafunzo ya siku tatu, yalioandaliwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Katibu Tawala Arusha,Katibu Tawala Msaidizi, Ufuatiliaji wa Menejimenti na Ukaguzi, Ramadhan Madeleka amesema mafunzo hayo yametolewa kwa wafanyabiashara hao kwaajili ya kufuata sheria .
Amewataka wafanyabiashara hao kufuata taratibu zote za usajili na upataji leseni wa biashara zao, ili zitambulike rasmi na kuepuka usumbufu wakati wa kazi zao.
Naye mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) , Isdor Nkindi amesema mafunzo hayo wanayatoa kwa wafanyabiashara wa mazao nje ya nchi ili waelewe umuhimu wa kurasimisha biashara zao na kupata leseni ili wafanye kazi kwa uhuru.
“Changamkieni fursa za kujikwamua kiuchumi ikiwemo kufanya biashara kwa urahisi kutokana na usajili wenu na sasa tupo hapa tumeweka kambi kwaajili ya usajili wa biashara zenu ili mfungue masoko ya biashara kwasababu mtatambulika kisheria”.amesema