Wafanyabiashara wa ndizi Murongo waahidiwa neema

MKUU wa mkoa Kagera, Albert Chalamila, amewahakikishia wafanyabiashara wa ndizi katika soko la Murongo kuwa,  serikali inawaandalia mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Chalamila alifanya ziara ya kutembelea soko la ndizi  la Murongo Wilaya ya Kyerwa na kupokea kero ya wafanyabiashara, ambao  wanauza ndizi zao katika mazingira yasoyoridhisha,  licha ya kuwa wanununuzi wakuu wa ndizi hizo wanatoka nchi jirani.

Sehemu wanayofanyia biashara hivi sasa ni eneo la mwenyeji mmoja, ambaye aliamua kutoa kwa muda, ili kuwasaidia wafanyabiashara wa ndizi Kyerwa, ambao miaka ya nyuma baadhi yao walikuwa wakienda kuuza ndizi zao nchini Uganda, huku wengine wakipata changamoto ya kudhulumiwa fedha zao.

Advertisement

Kutokana na hali hiyo, mwenyeji huyo, akaona atoe eneo hilo, ili wafanyabiashara  wa ndizi wapate kituo cha pamoja cha kuuzia ndizi na wafanyabiashara  kutoka nje waje kununua Tanzania na serikali ipate kodi.

Akizungumza jambo hilo, Chalamila alisema uongozi wa Mkoa wa Kagera, unajaribu kuzungumza na  viongozi wa Wizara ya Kilimo na kuwaomba watoe  soko lao la kimataifa lililoko Murongo, ambalo halijakamilika, ili wafanyabiashara hao wahamie hapo na kuondoka eneo walilopo sasa.

Mbunge wa Jimbo la Kyerwa, Inocent Bilakwate alisema uwepo wa  soko hilo katika mpaka wa Murongo,  umesaidia  kupanda kwa mkungu wa ndizi kutoka Sh1,500  hadi Sh  8,000

Alisema kipindi cha nyuma wafanyabiashara walinyanyaswa kwa kupeleka ndizi nchi jirani na baadhi  wakidhulumiwa fedha zao, hivyo kushindwa kuendelea na biashara, hivyo kumuomba Mkuu wa Mkoa kukamilisha mchakato na Wizara ya Kilimo ili soko hilo la kimataifa Murongo ambalo ujenzi wake umekwama likamilike.

Mtendaji wa Kijiji  Murongo, Datusi Noverth, alisema kuwa  kwa miezi 9 tangu soko la kuuza ndizi limeanzishwa,  tayari Kijiji cha Murongo, kimepata mgao wa Sh milioni 6, inayotokana na kukusanya ushuru, ambapo fedha hizo zimesaidia kujenga  matundu  manne ya vyoo vya kisasa katika shule ya msingi  Murongo.