Wasafirishaji: Muda wa ndege uzingatiwe kuhimili ushindani

WASAFIRISHAJI wa bidhaa za Tanzania nje ya nchi wameomba waendeshaji wa ndege ijayo ya mizigo kuzingatia muda, ili waweze kumudu ushindani katika masoko ya dunia.

Wametoa wito huo wakati wa mkutano wa kukusanya maoni ya wadau, uliondaliwa na shirika la ndege nchini (ATCL), juu ya nini kifanyike ili ndege hiyo ilete tija kwao na kwa nchi.

Ndege hiyo aina ya B767-300F inatarajia kuwasili nchini wiki ya pili ya mwezi huu na ina uwezo wa kubeba tani 54, amesema Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi.

Mhakiki Ubora Kampuni ya Victoria Perch, inayosindika minofu ya samaki, Edwin Okong’o, amesema inapotokea ndege ikachelewa hata kwa saa moja tu, tayari mteja wake huko nchi za Ulaya anapata hasara.

“Lakini hata sisi tunapoteza nafasi ya kushindana kibiashara. Mara zote mteja wetu anaendana na ratiba ya mnada wa siku husika huko kwao, ambayo ndiyo anayostahili kupokea mzigo ili auze ukiwa na ubora wake wa awali (fresh).

“Asipoupata kwa wakati inabidi asubiri siku nyigine ya mnada huku akiingia gharama za kuugandisha katika barafu, na bado hautauzwa ukiwa fresh,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa Mwanza, Adam Malima, amewataka wafanyabiashara wote Kanda ya Ziwa kuungana, kwa uhakika wa mzigo wa kujaza ndege hiyo.

“Mwanza peke yetu hatuwezi hata kidogo,” amesema.

Habari Zifananazo

Back to top button