Wafanyakazi TANESCO wachangia damu Mtwara
WAFANYAKAZI wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO), kwa kushirikiana na wananchi wengine mkoani Mtwara, leo wamejitolea damu kwa ajili ya kusaidia Mpango wa Damu Salama nchini.
Tukio hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya shughuli za wafanyakazi hao katika kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja iliyoanza jana Jumatatu.
Meneja wa TANESCO Mtwara, Mhandisi Tawakali Rwahila, amesema shirika hilo limekuja na mpango wa kuchangia damu kama sehemu yao ya kusaidia jamii.
“Wiki ya huduma kwa wateja imelenga kutoa elimu kwa kuwafuata wateja nyumbani, kuwapa huduma na kuwasikiliza, lakini pia kufanya jambo ambalo linagusa jamii kwa ukaribu sana la kuchangia damu,” amesema.
Mtaalamu wa utoaji damu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Mkoani Mtwara, Inosencia Charle ameshukuru wafanyakazi hao wa TANESCO kwa kutumia wiki ya huduma kwa wateja kujitolea kuchangia damu na kuhamasisha wananchi kuchangia pia.