HALMASHAURI ya Manispaa ya Ubungo mkoani Dar es Salaam, imewaagiza wafanyakazi wake kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa ueledi tofauti na ilivyo sasa.
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashim Komba ameagiza hayo wakati wa maadhimisho ya miaka 62 ya uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanywa na halmashauri hiyo.
Ameagiza walimu na maofisa ardhi kuwajibika katika nafasi walizonazo ili kutatua changamoto zilizopo katika taifa.
Pia amezungumzia suala la mmomonyoko wa maadili kwa kusema kuwa ili Tanzania iendelee kuwa salama lazima ihakikishe maadili yanalindwa.
” Matendo ya ulawiti, ubakaji yameanza kuonekana kama kitu cha kawaida siku hizi.
” Ndani ya wilaya ya Ubungo zipo kesi za watoto kulawitiwa, na kesi ya mzazi ambaye ni mlemavu, mtoto wake amelawitiwa,” amesema.
Ameviagiza vyombo vya usalama kuchukua hatua kali, kuhakikisha taratibu za upelelezi zinakamilika ili zifikishwe mahakamani,” alisema.
Ameonya tabia ya biashara ya kuuza mwili inayoshamiri kwa kasi.
“Tuna wajibu kupambana na kuchukia jambo hili. Kama taifa tukifika hatua ambayo watu wanazoea mambo ya ovyo tunafika pabaya.
Kila mmoja apambane na mmomonyoko wa maadili,” amesema.
Awali amesema kufikia miaka 62 ya uhuru sio jambo dogo kwani katika muda huo taifa limepitia mambo mengi, lakini amani ya nchi bado imekuwepo.
“Kuna mataifa mengine watu hawana uwezo wa kuabudu ama kufanya kazi kwa sababu mataifa yao yapo kwenye machafuko makubwa,” amesema.
Amesema katika kufikia miaka hii 62 ya uhuru watanzania wanatakiwa kuunganisha nguvu kumuombea Rais Samia Suluhu ili Tanzania iwe endelevu na imara.