Wafanyakazi wa majumbani waitwa Tuzo ya Mwalimu Nyerere

DAR ES SALAAM:.Wafanyakazi wa majumbani, Polisi pamoja na Wauguzi wameelezwa kujitosa katika Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, ambazo zinatarajiwa kutolewa Aprili 13 mwaka huu.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi, Machi 23,2014 na Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo hizo, Profesa Penina Mlama, alipokuwa akitangaza hatua ambayo uandaaji wa tuzo hizo umefikia.

Profesa Penina ambaye ni mwandishi wa siku nyingi wa vitabu , amesema jambo hilo limeonyesha uwepo wa mwitikio mkubwa wa tuzo hizo ambazo kwa mara ya kwanza zilitolewa mwaka jana.

,”Ushiriki wa kada nyingine katika tuzo hizi umetupa matumaini kuwa taarifa za tuzo hizo zimewafikia wengi hata wasio wanataaluma jambo litakalosaidia kuinua vipaji vipya katika uandishi wa fasihi na hivyo kuwa na uwanda mpana wa upatikanaji wa vitabu hivyo ambavyo kwa sasa ni vichache haswa vilivyoandikwa na watanzania,”amesema Mwenyekiti huyo.

Akizungumzia kuhusu tuzo hizo, amesema zitatolewa Aprili 13, ambayo ni siku aliyozaliwa Hayati Julius Nyerere huku akibainisha kuwa mshindi wa kwanza ataondoka na kitita cha Sh milioni 10 na kitabu chake serikali itakigharamia kukichapisha na kukisambaza mashuleni.

Kwa upande wa mshindi wa pili, atapata Sh  milioni 7 na watatu atapewa Sh milioni 5 huku washindi wa nne mpaka wa kumi watapewa vyeti kwa ajili ya kutambua ushiriki wao.

Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda, amesema mgeni anayetarajiwa kuja kutoa tuzo hizo ni Mshindi wa tuzo za Nobel kwenye uandishi wa Fasihi, Profesa Abdulazak Gurnah.

“Ushiriki wa Gurnah katika tuzo hizo kwetu kama nchi ni heshima kubwa kutokana na kujulikana duniani ,kwani kama mnakumbuka mwaka jana katika Tuzo hizi mgeni alikuwa Rais Mstaafu wa Msumbiji, Joachim Chissano ambaye ni Rais wa kwanza kuhutubia kwa lugha ya kiswahili katika mkutani wa Umoja wa nchi za Africa (AU),”amesema Waziri Mkenda.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ambao ndio waratibu wa tuzo hizo, Dk Anneth Komba, amesema shindano hilo ni endelevu na akiwataka watu kuendelea kuandika vitabu.

“Ni kwa kutambua umuhimu wa fasihi hata katika mitaala iliyoboreshwa serikali imeingiza somo la fasihi kwa watoto wetu hivyo vitabu vitahitajika, waandishi kazi ni kwenu kuandika vitabu vingi muwezavyo.

Aidha katika tuzo hizo amesema zaidi ya waandishi 400 kutoka ndani na nje ya nchi watahudhuria tukio hilo la utoaji tuzo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button