Wafariki wakichimba mchanga

WATOTO wawili wa familia moja wamekutwa wamefariki baada ya kufukiwa na mawe wakati wakichimba mchanga katika eneo la Maharahara kijiji cha Magata kata ya Magata Karutanga wilayani Muleba mkoani Kagera.

Diwani wa kata ya Magata Karutanga, Alhaji Yakubu Mahamudu alisema kuwa watoto hao walikuwa wanachimba mchanga Juni 26 asubuhi ndipo wakafukiwa na kifusi cha mawe.

Advertisement

Baada ya hapohawakuonekana nyumbani mama yao alitoa taarifa kwa uongozi na badaaye Wananchi walisaidiana na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuwatafuta sehemu ambayo kila siku wanajipatia riziki ndipo wakakutwa wamefunikwa na kifusi na wamefariki.

Yakubu aliwataja marehemu hao kuwa ni Samsoni Eliudi mwenye umri wa miaka 13 na Emmanuel Eliud mwenye umri wa miaka 10 ambapo wote walikuwa wanafunzi wa shule ya msingi Magata.

Alisema kuwa chanzo cha watoto hao kujihusisha na uchimbaji wa mchanga ni kujipatia kipato ambapo miaka iliyopita watoto hao walitelekezwa na baba yao mazazi na kubaki na mama yao pekee ambaye amekuwa akiwalea kwa kutafuta vibarua kwa wananchi na majirani huku akisaidiana na marehemu watoto wake.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Dk Abel Nyamahanga amedhibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusikitishwa na vifo vya watoto hao ambapo amepiga marufuku eneo hilo kutotumika kwa shughuli zozote za uchimbaji wa mchanga kutokana na mazingira hayo kutokuwa Rafiki kwa shughuli hiyo.

Aidha alitoa maagizo kwa viongozi wa vijiji na kata kukagua maeneo yote ya uchimbaji wa mchanga katika Wilaya hiyo ili kudhibiti maafa yasiweze kuendelea kutokea kwani shughuli za uchimbaji wa mchanga zimekuwa hazina mpangilio maalumu wala ukaguzi katika wilaya hiyo.

Baadhi ya wananchi ambao ni Ashimu Salimu na Godfrey Joel walisema kuwa tukio hilo limewasikitisha huku wakiomba kudhibiti vitendo vya baadhi ya wazazi kutelekeza watoto watoto wao kwani watoto wengi wamegeuka sehemu ya kujitafutia mahitaji ya familia baada ya kutekelezwa .

Jeshi la Polisi wilayani Muleba limefika eneo la tukio na kuruhusu taratibu za mazishi kuendelea.

1 comments

Comments are closed.