OFISI ya Ardhi Mkoa wa Katavi, imeanza mkakati wa kuwafuata wananchi kila kata hadi mtaa, lengo likiwa ni kuhakikisha kila mwananchi anayemiliki eneo au nyumba bila hati, anaipata.
Akizungumza wakati wa kupokea na kusikiliza kero za wananchi, ikiwemo kuwakamilishia hati wale wenye shida hiyo Kata ya Ilembo Manispaa ya Mpanda, Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Katavi, Geofrey Martin amesema kuwa, lengo la kuanzisha hatua hiyo ni baada ya kugundua wananchi wengi wanashindwa kufika ofisini licha ya kuwa na uhitaji huo.
“Baada ya kugundua wananchi hawa wamesumbuka kwa muda mrefu, tumeona na sisi sasa tuchukue jukumu la kuwafuata maeneo walipo na unaona kabisa mwitikio ni mkubwa,” amesema.
Amesema amebaini wapo baadhi ya wananchi walikuwa wameshalipia maeneo yao kwa zaidi ya miaka 10 na walikuwa hawajapata hati ya umiliki, hivyo watapatiwa hati ya umiliki kwa muda mrefu kutoka katika umiliki wa muda mfupi.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliojitokeza kupata huduma, wameushukuru uongozi wa ofisi ya Kamishna Ardhi Mkoa wa Katavi kwa kuendesha zoezi hilo, kwani mwanzoni walikuwa wanashindwa kurasimisha maeneo yao kutokana na uvivu wa kuzifuata ofisi zilipo ukizingatia pia umbali.
Shughuli hiyo imeanza katika Kata ya Ilembo na kwa mujibu wa maofisa hao wa ardhi itakuwa endelevu kwa maeneo yote ya Katavi.