Kundi la wafugaji 27 wamefariki dunia jana na wengine kadhaa kujeruhiwa katika kile polisi walichokiita mlipuko wa bomu katikati mwa Nigeria, eneo linalojulikana kwa mivutano ya kikabila na kidini.
Wafugaji hao na Ng’ombe walikuwa katika Jimbo la Nasawara kijiji cha Rukubi wakati tukio hilo lilipotokea katikati yao.
“Tumegundua watu 27 waliuawa katika mlipuko wa bomu pamoja na ng’ombe kadhaa,” alisema Maiyaki Muhammed Baba, Kamishna wa Polisi wa Nasarawa.
“Watu wengine walijeruhiwa na idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka kwani upekuzi bado unaendelea,” Baba alisema na kuongeza kuwa wataalamu wa mabomu wanachunguza chanzo cha mlipuko huo.
Kundi la mwamvuli linalowakilisha wafugaji lilisema kuwa bomu hilo lilirushwa na ndege ya kijeshi ya Nigeria.
“Lilikuwa shambulio la anga. Liliwaua watu wetu 27,” alisema Lawal Dano wa Muungano wa Wafugaji wa Ng’ombe wa Miyetti Allah wa Nigeria.
“Sote tunajua ni wanajeshi pekee wanaomiliki ndege kufanya mashambulizi ya angani, na tunatoa wito wa uchunguzi wa kina na kuwekewa vikwazo kwa yeyote anayehusika na hili,” Dano alisema.