BAADHI ya wafugaji wa kuku katika Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, wameacha kufuga kuku kutokana na hasara waliyoipata mwezi uliopita, ambapo kuku waliuzwa Sh 5800 hadi 6,000 badala ya Sh 6,700 hadi Sh 6,800.
Katibu wa Umoja wa Wafugaji wa Kuku wa Nyama Dar es Salaam na Pwani, Doreen Temu, amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo.
Temu amesema hasara hiyo imetokana na kuwepo kwa kuku wengi, ambao wafanyabiashara wa kuku na mawakala wa kuku, walitumia nafasi hiyo kuwakandamiza wafugaji kwa kutaka kuuziwa bei ndogo, ambayo haiendani na hali halisi ya gharama za ufugaji kwa sasa.
Pia amesema wafugaji wengi wamekata tamaa kwa sababu, kuna changamoto ya kupatikana kwa vifaranga nchini, lakini chakula kipo juu.
“Mwezi uliopita kuku walikuwa ni wengi, hivyo wanunuzi walitumia mwanya huo kuwakandamiza wafugaji kwa kutaka kuuziwa kwa bei ya chini, mfugaji naye kwa kuogopa kupata hasara zaidi aliwauza kuku kwa hasara,” amesema.
Kwa maelezo yake hivi sasa bei ya chakula cha kwanza cha kuku sh 80,000 hiyo ni ya jumla, reja reja ni sh 83,000 hadi 85,000, lakini mwanzoni kilikuwa sh 68,000.
Amesema chakula cha pili cha kuku bei ya jumla ni sh 79,000, lakini mwanzoni kilikuwa sh 62,000 na chakula cha mwisho ni sh 75,000, lakini mwanzoni kilikuwa ni sh 58,000.
Amesema upandaji wa chakula hicho unaelezwa kuwa ni kutokana na kupanda kwa malighafi ya kukitengenezea ambayo ni mahindi na soya.
Amesema pamoja na chakula hicho kuuzwa kwa bei kubwa suala la ubora wake nalo ni changamoto kwa kuwa kuku wa wiki mbili anakuwa anafanana na kuku wa wiki moja.