Wafugaji wa samaki wahakikishiwa mikopo

NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewahakikishia wanachama wa vikundi vya ufugaji samaki kwa njia ya vizimba mkoani hapa kupata mkopo wa Sh bilioni 2.5 mapema mwezi ujao.

Alitoa ahadi hiyo wakati akijibu hoja ya Mbuge Viti Maalumu anayewakilisha vijana, Ng’wasi Kamani, ambaye aliwasilisha changamoto ya vikundi hivyo kuomba mkopo zaidi ya miezi sita sasa kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo nchini (TADB), bila mafanikio.

Hoja hiyo iliwasilishwa mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa Naibu Waziri, wafugaji samaki na wadau mbalimbali wa uvuvi, uliolenga kujadili masuala kadhaa, ikiwemo jinsi ufugaji samaki unavyoweza kuchangia uchumi wa bluu.

Baada ya kusikia kilio hicho, Ulega alimuagiza Katibu Tawala Mkoa Mwanza kwenda Dodoma Alhamis ijayo na nyaraka zote za kuomba mkopo huo, ili kushughulikia suala hilo kwa haraka zaidi. “Hadi katikati ya mwezi ujao lazima mkopo uwe umetoka maana natambua tatizo lilipo kwa hawa watu wa benki ambao tutakua nao pia Dodoma,” alisema.

Alisisitiza kwamba ufugaji samaki ni wa muhimu kwani ndio utakaosaidia kukidhi mahitaji ya nchi ambayo ni tani kati ya 700,000 hadi 800,000 kwa mwaka, lakini zinapatikana tani 400,000 hadi 450,000. Alisema kutokana na umuhimu wa ufugaji huo, tayari wataalamu wameshafanya utafiti na kupata maeneo ndani ya Ziwa Victoria yanayotosha kuweka vizimba takribani 800.

Alisema mkoani Kagera nako tayari maeneo yamepatikana, muda si mrefu wataalamu wataelekea mikoa ya Mara, Simiyu na Geita. Ili ufugaji samaki uwe endelevu, mbunge aliiomba serikali kuwapatia wafugaji huduma ya bima ili kuwaepusha na hasara yoyote, ikiwemo majanga yanayoweza kupelekea vizimba kusombwa na maji.

Kero nyingine aliyowasilisha ni uwepo wa urasimu katika taasisi zote husika, za upatikanaji wa vibali vya kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa shughuli hiyo, changamoto ambayo Katibu Tawala Mkoa, Balandya Elikana, ahaidi kushughulika nayo ipasavyo.

Habari Zifananazo

Back to top button