Wafugaji wakorofi kutengwa

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imesema haitawaunga mkono wafugaji wakorofi na wasiofuata sheria zinazosimamia matumizi bora ya ardhi na watakao kusababisha  migogoro baina yao na watumiaji wengine wa ardhi wakiwemo wakulima.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo , Alexander Mnyeti  amesema hayo  wilayani Mvomero kwenye halfa ya uzinduzi wa kampeni ya Tutunzane Mvomero 2023 iliyozinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima.

Mnyeti amesema baadhi ya wafugaji wamekuwa wakitumia uwezo wao wa kifedha kutoa rushwa kwa baadhi ya watoa maamuzi wanapofikishwa kwenye vyombo vya haki licha ya  mkulima kupata hasara ya mazao yake kuliwa mifugo  huonekana ndiye mkosaji na kushindwa kupata haki yake.

“Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumeamua kusimamia ukweli na sheria  hatutakuwa tayari kumtetea mfugaji atakayevunja sheria na kuingiza mifugo  kwenye mashamba ya wakulima kwani kumtetea ni kuchochea migogoro ndani ya wilaya Mvomero na maeneo mengine  nchini .”amesema Mnyeti.

Mnyeti amesema  watoa maamuzi kutenda haki na kuepuka rushwa ili migogoro iliyopo Mvomero  na maeneo mengine nchini itoweke  na amani kwa jamii zote mbili itawale.

“Ni kweli  kuwa baadhi ya wafugaji ni wakorofi na wamekuwa wakiingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima kwa makusudi jambo ambalo halikubaliki.”amesema Mnyeti

Amesema ni vyema  wafugaji wa wilaya ya Mvomero na nyingine ndani ya mkoa huo kufuga mifugo yenye tija kwa taifa  na kujiepusha kutumia fedha walizo nazo kuwanyanyasa wakulima.

“ Wafugaji fungeni  mifugo yenye tija kwa Taifa, kulima mashamba ya malisho  pamoja na kuchimba visima vya kunyweshea mifugo. “ amesisitiza Mnyeti.

Mnyeti amesema kwa  kufanya hivyo kutachangia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya migogoro ya ardhi wilayani Mvomero na maeneo mengine nyakati za kiangazi.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mvomero, Judith Nguli amesema kampeni ya Tutunzane Mvomero 2023  imelenga kuleta ushirikiano ,umoja ,upendo na mshikamano baina ya wakulima na wafungaji hali ambayo itasaidia kwa kiwango kikubwa  kuondoa migogoro.

Habari Zifananazo

5 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button