MENEJA wa Kiwanda cha chanjo Tanzania kilichopo chini ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Charles Mayenga ameonya tabia ya wafugaji kutibu mifugo kiholela kwa kuwa inasababisha usugu wa vimelea vya magonjwa.
Mayenga ambaye pia ni daktari wa mifugo amesema hayo alipokuwa akizungumza na HabariLeo ofisini kwake na kueleza kuwa miaka ya karibuni kuwekuwepo na tatizo la watu kutibu mifugo bila kujua wanachotibu ni nini.
“Nasisitiza sana wafugaji kupima magonjwa ya mifugo kabla ya kuwatibu, ili kujua hakika tunakwenda kumtibu yule mgonjwa kwa dawa sahihi.
“Mchungaji anaamka asubuhi anakuta mifugo yake inaonesha haina afya nje anaingia ndani ana chupa yake ya dawa anavuta na kwenda kumchoma. Hapo hajui anatibu nini.
“Kwa hiyo tunajikuta dawa ile ile iliyokuwa inatibu ugonjwa fulani hivi sasa haiwezi kutibu, kwa sababu vidudu wamekuwa wakitibiwa pasipokuwa na utaratibu, hivyo wadudu hao ni wajanja sana unapopeleka dawa wao wanaisoma hiyo dawa ni ya namna gani halafu wanatengeneza kinga kuhakikisha kuwa haiwazuru, baada ya muda wanaizoea na mwisho haiwaui kwa sababu wamekuwa wamejua namna ya kuikwepa,” amesema.
Kwa maelezo ya daktari huyo, tatizo hilo limekwenda mpaka kwa binadamu, sababu wadudu ni wale wale ambao wanasababisha magonjwa na dawa ni zile zile zinazotibu binadamu ndizo zinazotibu wanyama.
“Matokeo yake kwa sababu na sisi tunakula yale mazao ya wanyama, unapokula mnyama ambaye alitibiwa na dawa zile zinaingia kwako kwa sababu zipo chini ya kiwango wadudu wale wale wanazizoea kwenye mwili wako na siku utakapougua ugonjwa kama huo ukienda hospitali na ukipewa dawa ile ambayo ilikuwa inakutibu kwa sababu wadudu wale wameshaizoea na kujenga usugu dhidi yake hautaweza kutibu,” amesema.
Kwa msingi huo amesema wakala hiyo inasisitiza wafugaji kutumia maabara zilizopo, ili kupata huduma hiyo ya kutambuliwa kwa magonjwa kabla ya kuyatibu, ili yakitibiwa kwa usahihi waondokane na hilo tatizo, lakini pia kuondokana na matumizi ya gharama kubwa katika matibabu yasiyokuwa na sababu.
Comments are closed.