WAFUGAJI nchini wametakiwa kuwa na utamaduni wa kuhifadhi malisho, ili kuweza kukabiliana na ukame unaotishia kuua mifugo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Idara ya mifugo Tixon Nzunda, wakati wa ziara ya kutembelea Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TARILI) na Taasisi ya Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA), kampasi ya Mpwapwa.
Nzunda aliwataka wafugaji kuwa na utamaduni wa kuhifadhi malisho ili kukabiliana na ukame.
Pia amezitaka taasisi zote za utafiti wa mifugo kuongeza kasi ya uzalishaji na uvunaji wa majani ya malisho, ambayo yatauzwa kwa wananchi, ili kuweza kutunza mifugo yao na kupata tija katika ufugaji wao.
Akizungumzia mradi wa uzalishaji wa ndama kwa kutumia viini tete, alisema wakati serikali inajipanga kuondoa changamoto zilizopo, lazima kuanza kufanya kile kinachowezekana kufanyika kwa kutumia raslimali zilizopo.
Kwa upande wake, Mtalaam wa kitengo cha maabara ya uzalishaji Kwa kutumia viini tete, Kabun Thomas alisema tayari wamefanikiwa kuzalisha ndama mmoja, ambaye ametokana na viini tete hivyo.
Alisema kuwa ili kukamilisha vifaa vyote vilivyobaki, taasisi hiyo inahitaji jumla ya Sh milioni 800, ili kukamilisha vifaa vyote vya kuvunia kugandishia na kuhifadhia, ili kuleta tija katika mradi huo.