Wafundwa uendeshaji mashauri ya watoto mahakamani

KIGOMA: WADAU 64 walio mstari wa mbele katika kushughulikia mashauri ya watoto mahakamani wanahudhuria mafunzo ya siku tano yanayolenga kuboresha uendeshaji bora wa mashauri ya watoto mahakamani ili hukumu zinazotolewa zizingatie ulinzi wa haki za mtoto kwa mujibu wa sheria za nchi na mikataba ya kimataifa ya haki za mtoto.

Mafunzo hayo yamefunguliwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma Augustine Rwizile ambaye ametaka wasimamizi wa kesi za watoto kuzingatia haki za mtoto kulingana na sheria na mikataba ya kimataifa inayolinda haki za Watoto ambayo serikali ya Tanzania imeridhia.

Jaji Rwize alisema kuwa uendeshaji wa mashauri ya mtoto yamekuwa na tofauti kubwa katika uendeshaji wake kulinganisha na mashauri mengine hivyo kumekuwa na changamoto mbalimbali kutoka kwa wadau kwenda pamoja katika kusimamia mashauri hayo hasa kwa watoto wanaokinzana na sheria.

Katika mafunzo hayo yanayoendeshwa na chuo cha uongozi wa mahakama Lushoto kwa ufadhili wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) Jaji Rwizile alisema kuwa chochote kinachofanywa katika kusimamia mashauri hayo kitapaswa kuzingatia sheria za nchi, sheria za kimataifa na mikataba ya kimataifa ya kumlinda mtoto ambayo Tanzania imeridhia.

Akizungumzia mafunzo hayo Afisa ulinzi na usalama wa mtoto kutoka UNICEF, Edna Lutengano alisema kuwa bado kumekuwa na changamoto kubwa kwa wadau wote katika kusimamia mashauri ya Watoto mahakamani kwanj wadau  wengi bado hawajui sheria na taratibu za kumlinda mtoto hasa wanaofanya makosa hivyo wadau wengi wanataka Watoto hao kushughulikiwa kama wahalifu wengine.

Nestory Kulula Wakili wa serikali kutoka ofisi ya Taifa ya Mwendesha mashitaka mkoa Kigoma alisema kuwa bado changamoto ipo kwa wadau wanaofungua mashitaka dhidi ya Watoto hivyo kutaka Watoto hao kushughulikiwa kama watu wengine wakati kuna tofauti kubwa ya uendeshaji wa kesi hizo.

Habari Zifananazo

Back to top button