MAOFISA afya na biashara wa halmashauri zote za Mkoa wa Mtwara wameshauriwa kutambua azma ya serikali ya kuhakikisha inakuwa na mtandao mkubwa unaoshughulikia udhibiti wa ubora na usalama wa chakula na vipodozi hapa nchini.
Ushauri huo ulitolea juzi na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Abdallah Malela, wakati akifungua mafunzo kwa maofisa afya na biashara wa halmashauri za Mkoa wa Mtwara.
Mafunzo hayo yalihusu sheria, kanuni na miongozo inayohusika na utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano baina ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Tamisemi.
Watumishi waliolengwa katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na TBS, ni maofisa afya na maofisa biashara kutoka katika ofisi ya mkuu wa mkoa, halmashauri za wilaya, miji, manispaa na majiji.
Aliwataka watambue kwamba azma ya serikali ni kuhakikisha inakuwa na mtandao mkubwa unaoshughulikia udhibiti wa ubora na usalama wa chakula na vipodozi.
“Kwa kulitekeleza hili serikali imeamua kuwatumia wakaguzi walio chini ya ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa katika shughuli za udhibiti wa bidhaa husika ili kulinda afya za watumiaji katika maeneo yao,” alisema Malel na kuongeza:
”Kwa kufanya hivi, itasaidia kuhakikisha shughuli za udhibiti zinafanyika kwa haraka na ufanisi zaidi,” alisema.
Aliwataka washiriki kufahamu kuwa sheria, kanuni na mwongozo zimepitia michakato yote inayotakiwa na zimepata baraka kutoka Tamisemi na Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.
“Hivyo watumishi wana wajibu wa kuelewa na kutekeleza makubaliano yaliyoainishwa kwenye sheria, kanuni na miongozo,” alisema.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Meneja Udhibiti Ubora wa TBS, Gervas Kaisi alisema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo watumishi na kuongeza ufanisi wa kazi.
“Lengo kuu la mafunzo haya ni kuwapa walengwa elimu kuhusu sheria, kanuni na miongozo inayohusika na utekelezaji wa majukumu ya ushirikiano baina ya TBS na Tamisemi,” alisema.
Alisema TBS imekuwa ikifanya shughuli za ukaguzi na udhibiti kwa kushirikiana na watumishi kutoka katika ofisi za halmashauri, hivyo anaamini mafunzo hayo yataongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yaliyoainishwa katika kanuni ya ushirikiano wa majukumu kati ya TBS na mamlaka za Serikali za Mitaa.
”TBS inatambua kuwa watumishi wa umma katika halmashauri za mikoa yote ya Tanzania hususani maofisa afya na maofisa biashara wana mchango mkubwa katika kulinda ubora na usalama wa bidhaa za chakula na vipodozi, ili kulinda afya ya walaji pamoja na kuleta tija katika uchumi,” alisema.