WAUMINI wa dini ya Kiislam kutoka mataifa mbalimbali, wameanza kuwasili mkoani Katavi katika ibada ya siku 3 ya Ijitimai ya kimataifa yenye lengo la kuendeleza amani na utulivu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Sheikh wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Kakulukulu, amesema Ijitimai ni ibada inayowakusanya waumini wa dini hiyo kutoka ndani ya nchi na nje ya nchi, ambapo mbali na kujengana kiimani, pia kutakuwa na dua mbalimbali na kwamba wanatarajia wageni 2000 watahudhuria Ijitimai hiyo.
Sheikh Kakulukulu amesema Ijitimai kufanyika katika Mkoa wa Katavi ni fursa kubwa kuutangaza mkoa, wafanyabiashara kujiingizia kipato, hivyo amewaomba wananchi wote kwa ujumla kujitokeza kuungana na waumini wa kiislam katika Ijitimai inayotarajiwa kuanza keshokutwa viwanja vya shule ya Sekondari Istiqama mjini Mpanda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Ijitimai ya Kimataifa, Amir Hassan Mwinyi, amesema wageni takribani 2,000 kutoka mataifa mbalimbali, wanatarajia kuhudhuria Ijitimai hiyo.