WANAFUNZI watatu wa familia moja, ambao wanasoma shule ya Msingi Makote wilaya ya Newala, mkoani Mtwara, wamelazimika kukaa nyumbani kwa miezi saba bila kuhudhuria masomo shuleni kutokana na mgororo kati ya Mwalimu Mkuu wa shule hiyo na baba mzazi wa watoto hao.
Mama wa watoto hao, Zainabu Daudi amemwambia Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas kuwa mmoja kati ya watoto hao ni mwanafunzi wa kike, ambaye alikuwa anasoma darasa la saba na alitakiwa kufanya mtihani wake wa mwisho, akashindwa baada ya kukaa nyumbani kutokana na mgororo huo.
Mama huyo anadai watoto hao walianza kukaa nyumbani mwezi Machi mwaka huu, baada ya baba wa hao watoto kushindwa kuelewana na mwalimu Mkuu kuhusu mchango wa shule, ambao uliitishwa na mwalimu huyo.
Alidai chanzo cha watoto hao ni babake kukasirika na kumwambia mwalimu Mkuu awafukuze shule na mwalimu huyo kuchukua uamuzi huo.
Akielezea mkasa huo, Ofisa Elimu Idara ya Elimu ya Awali Msingi Halmshauri ya Mji Newala, Mohammed Mwende amesema, shule hiyo ilitaka wanafunzi watoe mchango, lakini baadhi ya wazazi hawakukubaliana na suala hilo na kusababisha kuwepo kwa mfarakano ambao ulikosa suluhu kati ya wazazi hao na Mwalimu Mkuu.
Anasema baadae wazazi hao pamoja na Mwalimu Mkuu walikutana na kufanya kikao na Ofisa Mtendaji wa kata, kwa ajili ya kutafuta suluhu, ambapo ilionekana hao wazazi walikuwa na makosa.
“Baada ya kuonekana kuwa wazazi hao wana makosa walikubali wakaomba msamaha wa Mwalimu Mkuu, lakini mzazi wa watoto hao ambao kwa sasa hawaendi shule, hakutaka kuomba msamaha badala yake akawa mkali na kutaka kufanya vurugu kwa mwalimu Mkuu huyo,” amesema Mwende.
Amesema Baba mzazi wa watoto hao alienda shuleni akiwa na kisu akidaiwa kutaka kumchoma mwalimu Mkuu na Ofisa Mtendaji Kata.
Baada ya kusikiliza mkasa huo, Mkuu wa Mkoa Mtwara, Kanali Abbas, akamtaka Mkuu wa wilaya wa Newala, Mkurungezi pamoja na ofisa Elimu anayehusika kutatua huo mgororo kwa kuwaita wazazi na mwalimu Mkuu huyo na kuangalia chimbuko la mgororo huo na hatua zichukuliwe.
Pia amewataka viongozi kuhakikisha wanafunzi hao wanapelekwa shule haraka, ili haki yao ya kusoma isipotezwe.