Wagonjwa wa macho watakiwa kupata vipimo

MADAKTARI bingwa wa magonjwa ya macho wametoa angalizo kwa watu wenye matatizo ya macho kuacha kukimbilia kwenye nyumba za ibaada kuombewa badala yake wawahi kupata vipimo vya tatizo hospitalini.

Akizungumza kwa niaba, Daktari wa Macho mkoani Geita, Dk Anath Mussa amesema hayo wakati wa kliniki ya madaktari bingwa katika hospitali ya wilaya ya Bukombe iliyopo mji mdogo wa Ushirombo.

Dk Anath amesema tabia ya watu kukimbilia kuombewa na manabii wanapohisi changamoto ya macho kabla ya kujua nini kiini cha tatizo imesababisha tatizo kuzidi kukua na kupelekea wengi wao kupata upofu.

Aidha amewataka watu kuacha ulimbukeni wa matumizi holela ya dawa za kienyeji kwani pia imechangia kwa kiasi kikubwa watu kukuza matatizo ya macho ambayo huenda yangepimwa na kutatuliwa mapema.

“Wewe ukiwa kipofu, ni kipofu na familia yako, ina maana uchumi unayumba na familia yako, wewe mwenyewe inabidi ujitambue. Kwa hiyo tunaomba dawa za kienyeji pia msizitumie.

“Tumeshuhudia watu wengi kanisani, mtu ameumia au ameugua jicho anaenda kuombewa kanisani ikishindikana anakuta jicho tayari halina kazi.”

Ametahadharisha juu ya kukua kwa tatizo la mtoto wa jicho na presha ya macho na kuonya watu wanapohisi tatizo wasikimbilie kwenye maduka ya dawa kununua dawa za macho bila maelekezo ya daktari.

“Yaani watu wanachukulia jicho kama kitu cha kawaida, akiugua anaenda kuchukua dawa, lakini hiyo dawa pengine aliyoichukua inamuletea kupata tatizo kubwa ambalo hakuwa nalo.”

Daktari bingwa wa upasuaji kutoka Buchosa, Dk Sulusi Daniel ameongeza kuwa kasumba ya watanzania kutowahi vituo vya afya pia imepelekea wagonjwa wengi kuchelea kupata huduma ya upasuaji.

“Wagonjwa wanachelewa, wanafika kwa wakati ambao wamechelewa, hata namna ya utoaji matibabu sahihi kwetu inakuwa ni changamoto.

“Kwa kifupi tu ningeweza kuwashauri, unapoona kuna changamoto yeyote mwilini mwako chukua hatua haraka iwezekanavyo, njoo kwenye kituo cha kutolea huduma ili uweze kutibiwa.”

Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Said Nkumba amewataka wananchi kuzingatia ushauri unaotolewa na madaktari na kuacha kuishi kwa mazoea badala yake wafike vituo vya afya wanapohisi tatizo.

Habari Zifananazo

Back to top button