WATOA huduma kitengo cha mionzi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure, wamesema changamoto kubwa wanayokumba nayo ni wagonjwa kunyanyuka ghafla na kukimbia kutoka kwenye mashine, kwa hofu.
“Wanakurupuka wakati mashine imeshaanza kufanya kazi, hivyo kuvuruga mchakato na matokeo ya kipimo husika,” mtaalam wa mionzi, Dk Theresia Mabula, amesema leo na kuongeza:
“Akishavuruga kipimo kinarudiwa upya kwa sababu ni lazima tatizo linalomkabili mgonjwa na ukubwa wake lifahamike, ili apawe matibabu stahiki.
“Sasa changamoto ya kurudia kipimo mara kwa mara ni mionzi kuwa mingi kwa mgonjwa, ambayo baadhi ya madhara yake ni kusababisha saratani,” amesema na kufafanua kwamba:
“Watoa huduma wanajitahidi kutoa elimu na ushauri wakati wote kabla ya mgonjwa kuingia kwenye mashine, lakini bado changamoto hiyo ipo, hasa kwa wagonjwa ambao ni lazima wakae kwenye mashine takribani dakika 30.”
Amefafanua kwamba wanaolazimika kukaa muda huo ni wale wenye changamoto za kiafya kama vile uvimbe, matatizo kwenye mfumo wa chakula na katika mishipa ya damu, kwa sababu ni lazima wachomwe dawa itakayoelekeza tatizo liko wapi na ni kubwa kiasi gani.
Amesema wenye matatizo kama vile kuvunjika hawachomwi dawa, na muda wao kukaa katika mashine si zaidi ya dakika tano, amesema.
Pia amesema changamoto nyingine katika kitengo hicho ni wagonjwa kulazimisha kufanyiwa vipimo vya mionzi pasipo na ulazima.
“Elimu inaendelea kutolewa ili wananchi wajue madhara ya vipimo vya mionzi, ikiwemo kuharibu chembe hai za damu na kusababisha matatizo mengine kiafya,” mtaalam mwingine wa kitengo hicho Dk Tausi Mashaka amesema.
“Tunakua makini kuangalia ulazima wa kufanyiwa vipimo hivi na tuna vifaa vya kisasa kumkinga mgonjwa na mionzi ili isipenye sehemu nyingine za mwili, isipokua kwenye tatizo tu,” amesema.