Wahadhiri vyuo vikuu watakiwa kuongeza machapisho ya utafiti

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amewataka wahadhiri wa vyuo vikuu kuongeza machapisho ya tafiti katika majarida makubwa duniani ili kuweza kutambuliwa kama watafiti wabobezi.

Profesa Mkenda ameyasema haya jijini hapa wakati wa warsha ya kujadili na kutoa maoni kwenye rasimu ya Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na Kiunzi cha Uratibu wa Masuala ya Ubunifu.

Alisema hatua ya wahadhiri wa vyuo vikuu kuongeza machapisho ya tafiti katika majarida makubwa duniani kutafanya kutambuliwa kama watafiti wabobezi na kujipatia fedha hadi Sh milioni 50.

Alisema kwa sasa wahadhiri wengi wamekuwa waoga kufanya tafiti hasa za kisayansi.

“Hatutaweza kwenda kwenye maeneo yote kwa wakati mmoja, tunataka tuanze na utafiti wa elimu tiba, sasa hivi watu wanaogopa kufanya utafiti wa muda mrefu kutokana na ufinyu wa bajeti,” alisema.

Alisema kwa kutambua changamotoya kibajeti kwa watafiti, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetenga Sh bilioni moja ambapo kila mtafiti atakayekidhi vigezo atapata Sh milioni 50.

“Kwa ulimwengu wa sasa hauwezi kuepukana na masuala ya sayansi na teknolojia, hivyo nitoe rai kwa wadau wote kuchochea ubunifu kwa watoto ili baadaye waweze kujiajiri na kuajirika,” alisema.

Profesa Mkenda alisema misingi mingi imeshawekwa kwenye elimu na kuwa kwa sasa ni wakati wa kuweka uwezo wa kisayansi na teknolijia.

“Kuna misingi mingi tushajiwekea tusimame kwenye hiyo misingi badala ya kuanza upya na kurudi nyuma na kuzunguka na kurudi, kwenye elimu lazima twende mbali na bila elimu nzuri katika elimu hiyo tunataka tuongeze uwezo wetu katika sayansi uwezo, wetu katika teknolojia,” alisema.

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button