Wahalifu 76 wakamatwa Shinyanga
JESHI la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia watu 76 kwa tuhuma za kujihusisha na vitendo vya uhalifu ukiwemo wizi wa vifaa tiba boksi tano mali ya Serikali .
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, Janeth Magomi ametoa taarifa hiyo leo mbele ya waandishi wa habari ambapo amesema vifaa tiba hivyo vilikamatwa eneo la Nyamilangano Halmashauri ya Ushetu Wilaya ya Kahama.
Kamanda Magomi amesema vifaa tiba hivyo ni ‘gloves’ boksi tano ambazo zinatolewa na watumishi wa Serikali kwenye vituo vya huduma wasio waaminifu,ambapo amesema msako wa mara kwa mara utaendelea ili kukomesha vitendo hivyo.
Amesema vitu vingine vilivyokamatwa ni pamoja na bunduki moja aina ya Shortgun Pump Action yenye Namba za usajili Mv.95738V ambayo iliibiwa katika kijiji cha Mondo Wilaya ya Kishapu pamoja na vipande vya nondo 120.
Kamanda Magomi amesema wanaendelea kukabiliana na tatizo la wizi wa mafuta kwenye miradi mbali ya maendeleo ,ambapo wamekamata mafuta ya dizeli lita 100,pikipiki nane,betrii tatu za gari na kompyuta mpakato mbili.
Kamanda Magomi amesema wanaendelea kukabiliana na tatizo la uvutaji bangi na madawa ya kulevya ambapo katika msako na doria mbali mbali ndani ya mwezi mmoja wamefanikiwa kukamata pombe ya moshi lita 105,mirungi bunda 94,bangi kilo mbili na kete 10 na vifaa mbalimbali vya kupigia ramli chonganishi.