LUGHA ya Kichina hapa imeelezwa kuchochea ukuaji wa uchumi pamoja na kutoa ajira mbalimbali katika sekta binafsi na za umma hapa nchini.
Mwalimu wa lugha hiyo katika shule ya msingi na sekondari ya Baobao iliyopo jijini Dar es Salaam, Eliazary William, amesema hayo wakati wanafunzi wa shule hiyo, walipotembea na kujifunza utamaduni wa kichina katika taasisi ya Confucius, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
William amesema wanafunzi nane wa UDSM, waliosoma lugha ya kichina wameweza kuajiriwa mwaka huu kwenye fani za ualimu katika shule za serikali za sekondari na msingi pamoja na ukalimani katika lugha hiyo.
Kutokana na umuhimu katika lugha hiyo, ameshauri wanafunzi kuisoma lugha hiyo, ikiwa ni pamoja na shule kuweka utaratibu wa kufundisha.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Xiaozhen Zhang, amesema wapo kwa ajili ya kufundisha lugha ya kichina pamoja na utamaduni wake wa chakula, mavazi na michezo.
“Tunaamini katika kuonesha utamaduni wetu wa mavazi, chakula na michezo, wanafunzi wataipenda lugha ya kichina na kuelewa,” amesema.
Amesema taasisi hiyo haifundishi lugha peke yake, bali na utamaduni ili kila mmoja aweze kufahamu tamaduni za mwenzake na kumwelewa.
Mwanafunzi wa kidato cha kwanza Baobao, Grace Raphael ameshauri Watanzania wasome lugha hiyo kwa kuwa kwa sasa inajulikana ulimwenguni.