Wahamasishwa kulima ulezi kwa wingi

WAKULIMA nchini wamehamasishwa kulima ulezi kwa wingi, ili kuokoa fedha zinazopelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kununulia nafaka hiyo, kwa kuwa uliopo haukidhi mahitaji ya viwanda vinavyotengeneza unga lishe.

Mratibu kitaifa wa utafiti wa mazao ya mtama, uwele na ulezi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Ilonga kilichopo Kilosa Morogoro, Emmanuel Mwenda amesema hayo alipozungumza na HabariLEO kuhusu nafaka hiyo.

Amesema kwa kuwa soko lake hapa nchini halijawahi kuyumba na mahitaji yake ni makubwa, wenye viwanda wanaotengeneza unga lishe wa ulezi wanakwenda kununua nafaka hiyo nchini Zambia na Uganda, ili watimize malengo ya uzalishaji kwenye viwanda vyao kwa kuwa uliopo nchini hautoshelezi.

“Soko lake halijawahi kuyumba na mahitaji yake ni makubwa sana, tunavyo viwanda ambavyo vinatengeneza lishe kwa kutumia ulezi, uliopo Tanzania pekee hautoshi wanakwenda kununua ulezi Zambia na Uganda ili kutimiza malengo ya uzalishaji kwenye viwanda,” amesema.

Amesema pamoja na kwamba soko la nafaka hiyo halijawahi kuyumba, lakini uzalishaji wake unazidi kupungua mwaka hadi mwaka kwa sababu ya mazao mengine ambayo yameingia.

“Kwa mfano ukienda mikoa ya Kusini iliyokuwa ikilima sana ulezi sasa hivi imepungua kwa ajili ya kulima mazao mengine,” amesema.

Amesema ili kuhamasisha ulimaji wa nafaka hiyo, taasisi hiyo imetafiti mbegu mpya mwaka 2021 ijulikanayo kama TARIFM1, ambayo inazaa kwa wingi ikilinganishwa na mbegu mbili za awali zilizokuwa zimetolewa ambazo ni U15 na P224.

Amesema mbegu hiyo mpya ya TARIFM1 inazaa kuanzia tani tatu mpaka nne hivyo mkulima akifanya vizuri atapata magunia kuanzia 10 hadi 20 kwa ekari.

Naye Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Ilonga, Emmanuel Chilagani amesema kituo hicho kimepewa jukumu la kitaifa la kuratibu tafiti za mazao matano yakiwemo hayo ya mtama, ulezi na uwele.

Pia amesema kituo hicho kinatunza vinasaba kwa kupitia mbegu mbalimbali na sifa mbalimbali ambazo zinatumika katika ubunifu wa mbegu.

Habari Zifananazo

Back to top button