Wahamasishwa kuunganisha umeme Katavi

DIWANI wa Kata ya Ugalla na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Nsimbo, Mkoa wa Katavi, Halawa Malendeja, amesikitishwa na kitendo cha wakazi wa Kijiji cha Kasisi katika kata hiyo kushindwa kuunganisha umeme katika nyumba zao, wakati tayari umefika kijijini.

Alitoa kauli hiyo akizungumza na wakazi wa kijiji hicho katika Kitongoji cha Iseka kwenye mkutano wa hadhara wa kujadili maendeleo ya kijiji hicho na baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa katika Kijiji cha Kasisi na Kata ya Ugalla.

Amesema inasikitisha kuona umeme wa REA umefika kijijini kwao, lakini ni wananchi wawili tu ndio waliounganisha kwenye nyumba zao.

“Ndugu zangu wana Kasisi inatia aibu kweli, serikali imetumia gharama kubwa kutuletea umeme hadi hapa kijijini kwetu, tena wa gharama nafuu Sh 27,000 tu.

“Kweli tunashindwa kuweka mifumo ya umeme katika nyumba zetu na kulipia hizo gharama ndogo kabisa nyumba zetu zikawaka taa na serikali nayo ikaona kweli wameleta huduma sahihi kwa wananchi wao na kwa wakati sahihi? Amehoji Diwani Hawala.

Amewataka viongozi wa vitongoji, viongozi wa mashina wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) katika Kijiji hicho kuhakikisha wanatoa elimu na kuhamasisha wananchi wao kuvuta huduma hiyo ya umeme na kubadili maisha yao kwa kujenga nyumba za kisasa na kuhama kutoka nyumba za nyasi.

Habari Zifananazo

Back to top button