Wahimizwa kuacha maeneo uwekezaji nishati jadidifu

HALMASHAURI nchini zimeshauriwa kuona umuhimu wa kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa miradi ya nishati jadidifu, jambo litakalowarahisishia wawekezaji wenye nia ya kufanya hivyo.

Ushauri huo ulitolewa na Mkuu wa kitengo cha Mazingira, kutoka Wizara ya Nishati, Emillian Nyanda wakati akizungumza Dar es Salaam juu ya   mipango ya serikali katika kuhakikisha uwekezaji wa nishati jadidifu unafanyika nchini.

Alisema kwenye halmashauri nyingi nchini ni nadra sana kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji huo, hivyo kwa sasa ni muhimu kufanya hivyo ili utekelezaji ufanyike kwa haraka.

“Zipo baadhi ya halmashauri ambazo zimeanza kutenga maeneo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya nishati jadidifu ambazo ni pamoja na Same, Manyoni na Shinyanga. Kwa kufanya hivyo itasaidia wawekezaji kujua wapi kuna nini na kipi anaweza kufanyia wapi,” alisema.

Alisema ushauri huo unastahili ili kuongeza hamasa ya uwekezaji katika eneo hilo, na kila halmashauri ione umuhimu wa kutenga maeneo kwa ajili ya nishati jadidifu kwa kuwa uwekezaji wake unahitaji ardhi.

Aidha, alisema baada ya mwaka mmoja kuanzia sasa kutakuwepo na mtambo mkubwa wa kuzalisha umeme wa mwanga wa jua eneo la Kishapu, kwa megawati 150 na kwa kuanzia utazalisha megawati 50.

Kuhusu changamoto alisema ipo haja ya kuongeza uelewa kwa wafanya maamuzi kuhusu dhana nzima ya utekelezwaji wa nishati jadidifu nchini na kwamba ni muhimu kuelewa kuwa suala hilo ni mtambuka likihusisha kila sekta.

Habari Zifananazo

Back to top button