Wahimizwa matumizi ya vyandarua

WAKAZI wa Kijiji cha Nakapanya, Halmashauri ya Wilaya Tunduru mkoani Ruvuma, wamekumbushwa umuhimu wa kutumia vyandarua vyenye viuatilifu na kudumisha usafi wa mazingira kwenye maeneo wanayoishi kuepuka mazalia ya mbu wanaoeneza malaria.

Wito huo ulitolewa jana na Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa, Abdallah Shaib Kaim, wakati akizindua ugawaji wa vyandarua kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wajawazito wilayani Tunduru.

Aliwataka wananchi kuachana na imani potofu kuwa vyandarua vyenye dawa ni hatari kwa afya zao na kuwahakikishia kwamba vimetolewa na serikali, ni salama na havina madhara kwa binadamu.

Kaim ameonya wakazi wa Wilaya ya Tunduru kutumia vyandarua hivyo kwa ajili ya bustani, kufugia mifugo na kuvulia samaki, badala yake watumie kujikinga na maambukizi ya malaria hasa usiku.

Alipongeza Wilaya ya Tunduru kwa jitihada inazofanya katika kutokomeza ugonjwa huo unaotajwa kuwa ni kati ya magonjwa hatari na yanayoongoza kupoteza maisha ya watu wengi nchini.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Tunduru, Chiza Marando alisema serikali kwa kushirikiana na wahisani Global Fund imetumia Sh 54,280,000 kununua na kusambaza vyandarua vyenye dawa.

Kwa mujibu wa Marando, kuanzia mwaka 2020 hadi Machi mwaka 2023, halmashauri hiyo imegawa zaidi ya vyandarua 176,747 kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na wajawazito kama mkakati wake wa kukabiliana kuenea kwa ugonjwa wa malaria.

Marando alisema mwaka 2020 waligawa vyandarua 51,409, mwaka 2021 vyandarua 60,792, mwaka 2022 vyandarua 59,847 na hadi kufikia Machi 30, mwaka huu wametoa vyandarua 4,699.

Alisema kutokana na jitihada na mikakati inayofanywa na halmashauri hiyo, takwimu za wagonjwa wa malaria zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka kutoka wagonjwa 102,628 mwaka 2020/2021 sawa na asilimia 44 ya wagonjwa 228,991 waliopimwa ugonjwa huo hadi wagonjwa 81,248 mwaka 2021/2022.

 

Habari Zifananazo

Back to top button