VIJANA waliohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria, wametakiwa kufichua makundi ya uhalifu wakiwemo vijana wahalifu wanaojiita panya road.
Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Remedius Mwema wakati wa kuhitimisha safari ya mafunzo ya miezi mitatu ya Operesheni Jenerali Venance Mabeyo kwa vijana wa Mujibu wa Sheria katika kikosi cha 834 JKT Makutupora.
Alisema vijana wanapaswa kuwa wazalendo na kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kushirikiana na serikali katika kuibua na kufichua vitendo vya kihalifu ili nchi iwe salama.
Naye Mwakilishi wa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kanali George Kazaula amewataka vijana hao kuendelea kuishi kwenye viapo vyao.
Alisema JKT inaendelea kuamini kuwa kiapo cha utii ambacho wamekiapa ni ishara tosha kuwa taifa limewekeza sehemu sahihi.
Kamanda Kikosi 834 JKT Makutupora, Luteni Kanali Festo Mbanga alisema vijana hao wamejifunza mafunzo ya awali ya kijeshi ambayo yamewafanya wawe wajasiri, hodari na utimamu wa mwili.