PWANI; VIJANA wanaohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wa kujitolea, wametakiwa kutumia dhana ya uzalendo katika shuguli za ujenzi wa Taifa, ili kuiletea nchi maendeleo.
Hayo yamesemwa Mlandizi, Pwani na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John wakati wa kufunga mafunzo ya (JKT) ya kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT kwenye Kikosi cha Ruvu Kibaha.
Amesema vijana hao wameandaliwa vyema kulipambania Taifa, hivyo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao lazima watangulize uzalendo.
“Zingatieni mambo manne muhimu utii, nidhamu, uhodari na uaminifu haya ndiyo mambo ya kuzingatia hapa ndipo mtakuwa mnafanya uzalendo ambayo ndiyo nguzo kuu ya mafunzo yenu,”amesema John.
Amesema pia wawe na uhodari kwenye jambo moja ambalo ni fani, ili wawe mahiri kwani kuchanganya mambo mengi kwa wakati mmoja hawataweza kuwa mahiri.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi, Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema kuwa vijana hao wanapaswa kujilinda kiafya kwani suala la afya ni muhimu sana.
Mhona ambaye pia ni Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kuwa mafunzo hayo ni ya kuwapatia stadi za maisha na baadaye watapata stadi za kazi ikiwa ni hatua ya pili baada ya hatua ya kwanza.
Amesema mafunzo hayo yamekuza moyo wa uzalendo ukakamavu na kutumia vizuri muda na hawajakosea kujiunga na mafunzo hayo ya kujitolea, kwani maamuzi yao ni ya busara na kuwapongeza wazazi na walezi kwa kuwapeleka vijana wao kwenye mafunzo hayo.
Naye mwakilishi wa Mkuu wa JKT, Kanali Robert Kessy amesema wakati wa kutekeleza majukumu yao wahakikishe wanatatua changamoto bila kuvunja sheria na kuwa na nidhamu bila kusahau uhodari, kwani Taifa limewekeza sehemu sahihi.
Amesema kuwa vijana wanapaswa kujitolea kulitumikia Taifa na kumuenzi Baba wa Taifa, ambaye aliasisi Jeshi hilo na wahakikishe wanaonesha uzalendo kwa vitendo na weledi na wajiulize watalifanyia nini Taifa siyo Taifa kuwafanyia nini, pia wahakikishe wanasimamia viapo vyao.
Awali Mkuu wa Kikosi cha Ruvu 832 KJ Kanali Peter Mnyani ,alisema kuwa mafunzo hayo ya awali ya kijeshi waliyoyapata vijana hao ni pamoja na ukakamavu ujasiri ambavyo wamefanya kwa vitendo.
Amesema mafunzo hayo yalikuwa ya muda wa miezi minne kati ya miezi 24 ya mkataba wao, ambapo walijifunza utimamu wa mwili, usomaji ramani, uraia, usalama na utambuzi na kwata za silaha ndogo ndogo.
Akisoma risala ya wahitimu wa mafunzo hayo Lulu Godfrey alisema kuwa Vijana wa Kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT walianza mafunzo hayo Desemba 2023.
Godfrey alisema kuwa kwenye mafunzo hayo walifundishwa mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja mbinu za ulinzi, ukakamavu, utii, ulinzi wa taifa ujasiri uvumilivu, na hawatatumia vibaya mafunzo hayo kinyume na malengo ya Taifa.
Jumla vijana 800 walijiunga na mafunzo hayo ambapo waliohitimu walikuwa 776 wavulana wakiwa 438 na wasichana walikuwa 338 na vijana 24 hawakumaliza mafunzo hayo na kwa kipindi cha miezi 20 watakuwa kwenye majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na malezi, uzalishaji mali na ulinzi.