MWANZA; Magu. Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Jubilate Win Lawuo, amewataka wahitimu wa mafunzo ya mgambo wilayani humu kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri, ili waweze kujikwamua kiuchumi mara baada ya kuwa wamehitimu mafunzo yao.
Akifunga mafunzo hayo yaliyodumu kwa miezi minne katika viwanja vya Msalaba Mwekundu vilivyopo Kata ya Kisesa, Lawuo amesema kuwa si vyema vijana hao kusambaratika mara baada ya kuwa wamehitimu mafunzo hayo ya mgambo, badala yake watumie fursa mbalimbali zilizopo katika Wilaya ya Magu.
“Pale katika halmashauri yetu ya Wilaya ya Magu tunawezesha vijana kama nyie kwa kuwapa mikopo, mara baada ya kumaliza mafunzo nendeni mkatengeneze vikundi halafu mje halmashauri tutawawezesha kupata mikopo ambayo naamini kwa namna moja au nyingine itawasaidia kujikwamua kiuchumi, “amesema.
Pia Lawuo amewataka wahitimu hao kwenda kuishi ndani ya viapo vyao, baada ya kumaliza mafunzo hayo, huku akitoa pongezi kwa wakufunzi wa mafunzo hayo kwani wamefanya kazi kubwa na nzuri.
Kwa upande wake mshauri wa Jeshi la akiba wilayani Magu, Gadiel Charles amesema kuwa wanafunzi waliofanikiwa kuhitimu ni 68 kati ya wanafunzi 93 walioanza mafunzo hayo na wengine walipungua kwa namna mbalimbali ikiwemo baadhi ya wanafunzi kujiunga na Jeshi la kujenga Taifa (JKT).
Comments are closed.