Wahitimu UDSM wahimizwa amani

DAR ES SALAAM: MAHAFALI ya 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), jumla ya wahitimu 2,046 kutoka ngazi mbalimbali za masomo walitunukiwa vyeti na shahada zikiwemo Shahada ya Uzamivu, Shahada ya Umahiri, Stashahada ya Uzamili, Shahada ya Awali, Stashahada na Astashahada.

Sherehe hizo zilizofanyika jijini Dar es Salaam, zilitawaliwa na ujumbe wa kuhimiza vijana kulinda amani, kuendeleza mshikamano na kuutumikia vyema ujuzi walioupata kwa manufaa ya taifa.

Akizungumza katika mahafali hayo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye alisema uhai, usalama na maendeleo ya taifa lolote duniani yanategemea nguvu ya vijana, hivyo ni wajibu wao kutumia ujana kwa manufaa ya jamii.

“Hakuna asiyejua mchango wa vijana katika Taifa. Tumieni ujana wenu kwa faida na msichoke kulinda amani popote mlipo,” amesema Prof. Anangisye.

Amesisitiza kuwa elimu waliyoipata inapaswa kuonekana kwa vitendo kwa kuitumikia jamii kwa kuzingatia sheria, maadili na miongozo ya nchi.

Aidha, aliwashauri vijana kuwa tayari kutumia ujuzi wao katika maeneo mbalimbali hata pale fursa za ajira katika serikali au sekta binafsi zinapochelewa kupatikana.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Mrisho Kikwete, amesema ana faraja kuona ongezeko la wahitimu wa elimu ya juu, hususa wa ngazi ya uzamivu.

Amewataka kutumia elimu yao kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Katika mahafali hayo, jumla ya 65 walitunukiwa Shahada ya Uzamivu (PhD), wakiwemo wanaume 45 na wanawake 20, sawa na asilimia 30.8 ya wahitimu wa ngazi hiyo.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Balozi Mwanaidi Maajar, amewataka wahitimu kwenda kuthibitisha taaluma zao kwa vitendo na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.

Amesisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuendeleza misingi bora ya malezi, hasa kipindi hiki cha utandawazi, ili kuepusha kizazi tegemezi kisichoweza kuwajibika.

Idadi ya wahitimu kwa mujibu wa ngazi za masomo katika duru ya nne ya mahafali ya 55 ni kama ifuatavyo: Shahada ya Uzamivu (PhD): 65 Shahada ya Umahiri (Masters): 522
Stashahada ya Uzamili (Postgraduate Diploma): 26 Shahada ya Awali (Bachelor’s): 1,291 Stashahada (Diploma): 126 Astashahada (Certificate): 16

Kwa ujumla, wahitimu wametakiwa kuwa mabalozi wazuri wa amani, maadili na maendeleo ya taifa wanapoanza safari mpya katika maisha yao ya kitaaluma na kijamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button