Wahitimu vyuo vya ufundi watakiwa kufikiria kujiajiri

WAHITIMU wa vyuo mbalimbali vya ufundi stadi wilayani Singida vimeshauriwa kuachana na dhana ya kuajiriwa badala yake wafikirie zaidi kujiajiri ili waweze kufikia malengo yao ipasavyo.

Rai hiyo ilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Singida, Paskasi Muragili kwenye mahafali ya wahitimu wa kozi fupi ya ufadhili wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika Chuo cha Ufundi Stadi na Marekebisho kwa watu wenye ulemavu Sabasaba mjini Singida.

Alisema kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ana nia ya dhati na wananchi wake wasio na kipato, hasa vijana, wanawake na wenye ulemavu, amepeleka fedha nyingi kwenye halmashauri za wilaya, miji na manispaa ili wasio na kipato waweze kwenda kukopa na kujiendeleza.

“Mnachofanya hapa ni cha kiwango cha hali juu. Tatizo ni mitaji, changamoto ambayo ni ya muda mfupi tu. Mkijipanga vizuri, mkajitambua, mkajiamini kuwa mnaweza na mkawa tayari basi mtafanikiwa,” alisema Muragili.

Aliwataka wahitimu hao kwenda kwenye halmashauri zao kuomba mikopo itakayowasaidia kujikwamua na hatimaye kujiimarisha kiuchumi hata kufikia hatua ya kuajiri wengine.

“Hapa mmepewa maarifa, jiongezeni kwa kuwa wabunifu zaidi kulingana na soko lilivyo. Lakini pia changamkieni fursa za mikopo iliyoletwa na Mama Samia kwenye halmashauri zenu.

Hiyo ni fursa kubwa kwenu, itumieni,” alisema. Muragili alizishauri halmashauri kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo ya vitu badala ya fedha taslimu ili kuepuka upotevu usio wa lazima wa fedha zinazokopwa ambapo baadhi ya wanaokopa hushindwa kurejesha.

Awali katika risala iliyosomwa kwa niaba yao na Yustina Kidua pamoja na mambo mengine, wahitimu hao waliiomba serikali iwapatie nafasi za ajira kwenye ofisi zake mbalimbali nchini kulingana na ujuzi wao.

Mkuu wa Chuo hicho, Fatuma Malenga alieleza kuwa chuo hicho kilichoanzishwa mwaka 1977 kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na ya Sweden ikiwa ni sehemu ya huduma za marekebisho kwa watu wenye ulemavu, kinapokea wanafunzi kutoka mikoa yote wenye umri wa miaka 15 hadi 35; wakiwemo watumishi wa umma ambao wamepata ulemavu kazini.

Alisema mipango ya baadaye ni kuanzisha mafunzo ya muda mfupi ya lugha ya alama kwa watumishi ili waweze kuhudumia wateja wenye ukiziwi na kuanzisha kituo atamizi kitakachojikita katika kutoa uzoefu wa uzalishaji kwa wanafunzi kulingana na fani walizosomea. Kadhalika kuwa na kituo cha rasilimali kwa watu wenye ulemavu nchini kwa upatikanaji huduma za upimaji na utoaji vifaa saidizi kwa kundi hilo chuoni na nje ya chuo.

Habari Zifananazo

Back to top button