Wahofu ongezeko mbwa wenye vichaa

WAKAZI wa mamlaka ya mji mdogo wa Katoro wilayani Geita wameiomba serikali kusaidia kudhibiti mlipuko wa ugonjwa wa kichaa cha mbwa kutokana na ongezeko la watu waliong’atwa na mbwa wanaosadikika kuwa na kichaa eneo hilo.

Wakizungumza na waandishi wa habari juzi, walisema kwa sasa kuna idadi kubwa ya mbwa wanaozagaa bila makazi maalumu mtaani na tayari kuna watu wawili wanasadikika kufariki kwa ugonjwa wa kichaa cha mbwa.

Ezekiel Emmanuel, mkazi wa Kitongoji cha Kalifoni, Kata ya Ludete alisema kijana wake mwenye umri wa miaka 20 alifariki kwa tatizo hilo hivi karibuni baada ya kung’atwa na mbwa mwenye kichaa.

Naye, Janeth Godfrey alisema tatizo hilo ni tishio kwani watoto, vijana na watu wazima wa eneo hilo hawana amani kutembea mtaani kuanzia asubuhi, mchana hadi jioni kwani mbwa wenye tatizo hilo ni wengi.

Ofisa Mifugo na Uvuvi, Kata ya Ludete, Joachim Kamajura alikiri tatizo la mbwa kuzagaa mtaani ni kero kubwa kwani mbwa wanaozurura ni wengi kuliko wanaomilikiwa na wananchi kwa ajili ya ulinzi.

Alisema ndani ya mwezi Desemba, 2022 amepokea taarifa za watu sita kung’atwa na mbwa na miongoni mwao wawili wamefariki dunia ingawa hawajathibitishwa kufariki kwa kichaa cha mbwa.

Kaimu Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Katoro, Dk Zakaria Shija alisema kuanzia Septemba hadi Desemba 7, 2022 wamepokea na kutoa chanjo kwa watu 54 waliolalamika kung’atwa na mbwa wanaodhaniwa kuwa na kichaa cha mbwa.

Habari Zifananazo

Back to top button