Waiomba Latra kuharakisha ratiba ya mabasi

WATUMIAJI wa huduma za usafiri wa mabasi nchini wameiomba Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuharakisha utaoaji wa ratiba itakayoyawezesha mabasi kutoa huduma za kwenda mikoani kwa saa 24 .

Kauli ya wadau hao hususani abiria pamoja na Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) imekuja siku chache baada ya serikali kuruhusu huduma za usafiri wa mabasi hayo kutolewa kwa saa 24 ikisisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza uchumi wa nchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Jijini Dar es Salaam, wadau hao akiwemo mfanyabiashara wa mazao katika soko la Kariakoo Benson Maona na mwananchi mwengine aliyejitambulisha kwa jina la Maimuna Ibrahim, wamesema kwa kufanya hivyo pamoja na mambo mengine kwa kiasi kikubwa kutasaidia kutatua tatizo la usafiri nchini.

Akizungumzia kuhusu hilo, Maona amesema kwa kipindi kirefu hususani nyakati za msimu wa sikukuu kumekuwa kukijitokeza tatizo kubwa la usafiri wa kwenda mikoani na kuongeza kuwa hatua hiyo ya serikali kuruhusu huduma kwa saa 24 kunaenda kumaliza kabisa tatizo hilo.

“Tunamshukuru Waziri Mkuu kwa kutamka Bungeni hatua ya Serikali kuruhusu huduma za mabasi kwa Saa 24, hatuoni sababu gani zinazozuia huduma hiyo kutolewa hadi muda huu, Mamlaka yenye dhamana ya usimamizi wa usafiri (LATRA) ione uzitoa wa kauli ya Waziri Mkuu kwa kutekeleza haraka suala hilo” amesema Maona

Kwa upande Maimuna mbali na kuipongeza serikali amesema ni vyema Latra ikaharakisha suala hilo ili kuondoa kabisa changamoto ya abiria kulazimika kupanda magari ya mizigo yakiwemo malori hususani nyakati za usiku pale wanapopatwa na dharura mbalimbali na kulazimika kusafiri kwenda mikoani.

“Hivi sasa tunaona ratiba za mabasi zinaanza kuanzia Saa tisa usiku, bado haikakidhi matakwa yetu kama abiria, kuna wengine tunatokea maoneo ya vijijini hivyo kuwepo kwa ratiba ya saa 24 kutatusaidia kupanga vizuri muda wa kusafiri ili kufika tuendako kwa muda unaostahili Latra, serikali iliona mbali kutaka ratiba za mabasi ziwe ndani ya muda wote mchana na usiku” amesisitiza Maimuna

Awali Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) kupitia kwa Mwenyekiti wake Abdallah Mohamed amesema waliopokea kwa uzito mkubwa kauli ya Waziri Mkuu ya mabasi kutembea kwa saa 24 na kwamba wao kama wasafirishaji walishajipanga na suala hilo hivyo wanasubiri ratiba kamili itolewe na LATRA.

“Tunaishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukisikia kilio chetu cha muda mrefu kwa kuturuhusu kutoa huduma za usafiri kwa Saa 24, ukweli kama nchi tulichelewa kutoa huduma hiyo kutokana na kuwa na manufaa mengi hasa katika eneo zima la ukuaji wa uchumi wa Taifa letu” amesisitiza.

“Aidha pamoja na Shukrani zetu kwa Rais Samia sisi kama wasafirishaji pia tunapenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson kwa kulisimamia suala hadi leo hii tulipofika hapa, ukweli tunawashukuru sana viongozi wetu hawa kwa kuzingatia maslahi ya taifa” ameongeza.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button