WAKAZI wa kijiji cha Majengo kata ya Namtumbuka Halmashauri ya Mji wa Nanyamba mkoani Mtwara wameiomba serikali kuwajengea kituo cha afya ili waondokane na changamoto ya kwenda maeneo jirani kufata huduma hiyo.
Ombi hilo limetolewa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoadhimishwa katika halmashauri hiyo.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo Machi 7, 2024 yenye kauli mbiu inayosema ” Wekeza kwa Wanawake Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Ustawi wa Jamii”
Mkazi wa kata hiyo, Rehema Nayopa amesema zahanati wanayo katani humo ila changamoto kubwa ni ukosefu wa kituo cha afya.
“Tunaishukuru serikali kwa kuwa huduma za afya tunapata katika zahanati yetu lakini bado tunaomba itujengee kituo cha afya kwasababu sisi akina mama tunapata changamoto wakati wa kujifungua kutoka hapa kwenda vijiji jirani”
Diwani wa Viti Maalum wa kata hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Sofia Champunga amesema kata hiyo ina vijiji vinne ambapo kwa sasa wakazi hao wanaenda kata ya Dinyecha, Kilomba kwenye halmashauri hiyo kufata kitu cha afya.
“Wanatembea umbali kadhaa kufata kituo cha afya, baadhi ya akina mama wajawazito wanakuwaga na changamoto wakati wa kujifungua sasa kutokana na umbali huu wapo ambao walijifungulia njiani,” amesema Champunga
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Maliki Hamisi ameielekeza halmashauri kwamba fedha zozote zitakazoletwa kwenye halmashauri hiyo wajenge kituo cha afya katani humo ili kuwaondolea adha hiyo wakazi hao.
Aidha, maadhimisho hayo yameambatana na utoaji wa msaada kwenye sekta mbalimbali ikiwemo kitanda cha wagonjwa kimoja kilichotolewa katika zahanati ya Namtumbuka iliyopo katika kata hiyo.
Pia zimetolewa taulo za kike kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi wa kike kwenye shule mbalimbali za sekondari katika halmashauri hiyo.
Aidha mgeni rasmi wa maadhimisho hayo ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Mtwara, Mwajuma Nahembe.