Waishio na VVU wataka usawa huduma muhimu

BARAZA la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini (NACOPHA) linahitaji kuimarisha usawa katika upatikanaji wa huduma muhimu wakati huu ambapo dunia inaadhimisha Siku ya Ukimwi.

Desemba mosi kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Ukimwi ili kuongeza ufahamu kuhusu Ukimwi na kuwakumbuka wote waliopoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.

Hoja ya NACOPHA inakwenda sambamba na kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema: ‘Imarisha Usawa’ ambayo inakumbusha kuzingatia ushirikishwaji wa watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (WAVIU) kutoka makundi yote ya kijamii katika kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wote nchini ili kuyafikia malengo ya 95- 95- 95.

Taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Nacopha, Leticia Mourice ilisema: “Namba 95-95-95 inalenga kuhakikisha kuwa asilimia 95 ya Watanzania wawe wametambua hali zao za Virusi Vya Ukimwi (VVU); 95 wawe wamewekwa katika huduma ya tiba na 95 wawe wamefanikiwa kufikia hali ya mfubao wa virusi vya Ukimwi kwenye damu ifikapo mwaka 2025.”

Alisema maadhimisho ya mwaka huu yamekuja wakati ambapo idadi ya wanaume, wanawake, wavulana na wasichana wanaopata huduma muhimu za matibabu na mitaji ya kuwasaidia kiuchumi imeongezeka.

Aliishukuru serikali kwa kufanya kazi pamoja na mashirika ya kiraia na wadau wa maendeleo ambapo alisema idadi ya vijana wanaoishi na virusi vya Ukimwi ambao wamepatiwa mafunzo ya ufundi na ujasiriamali na kisha kupewa mitaji ya kuendesha biashara zao kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu nayo imeongezeka.

Nacopha ni asasi ya kiraia inayoundwa na watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi kupitia vikundi wezeshi na Konga za Waviu Tanzania Bara.

Kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, hadi sasa Nacopha ina Konga za Waviu katika halmashauri 184 za Tanzania Bara na wanachama wapatao 666,022, wanawake 423,058 na wanaume 242,964.

Asilimia 44 ni ya Waviu wote waliosajiliwa kwenye Mpango wa Taifa wa Tiba na matunzo walio zaidi ya miaka 18 na wote wanatumia dawa.

Hivi sasa Nacopha inatekeleza mradi wa Hebu Tuyajenge 2019-2024 kwa ufadhili wa Watu wa Marekani. Mradi huu unalenga kupunguza kasi ya maambukizi ya virusi vya Ukimwi na malengo ya kitaifa ya kufikia 95-95-95 ifikapo mwaka 2025.

Habari Zifananazo

Back to top button