WANANCHI wa Kijiji cha Amani wilayani Newala mkoani Mtwara wameishukuru serikali kwa kuwaletea mradi wa nyumba ya watumishi wa afya kwenye zahanati iliyopo kijijini hapo uliyogharimu zaidi ya Sh milioni 50.
Akizungumza leo wakati mbio za Mwenge wa Uhuru ulipotembelea mradi huo na kuweka Jiwe la Msingi, mwenyekiti wa kijiji hicho, Athumani Hassan amesema uwepo wa nyumba hiyo utasaidia watumishi wa zahanati hiyo kufanya kazi vizuri na kutoa huduma kikamilifu.
“Tunaishukuru Serikali inavowaboreshea mazingira mazuri ya ufanyaji kazi hawa wataalam wetu inawapa hamasa kubwa kuweza kutuhudumia sisi wananchi kwa moyo mmoja na kujituma katika utendaji wao wa kazi”,amesema Hassan
Adina Hamisi mkazi wa kijiji hicho amesema ” Tumefurahishwa sana kuona Serikali imewajali madaktari wetu tunajua watafanya haki kutuhudumia vizuri sisi wananchi wakati tunapoenda Zahanati kupata huduma ya afya ila tunaiomba Serikali uboreshaji huu usiishie hapa tu kwenye Zahanati hii tu iwe hata kwa maeneo mengine ili wananchi tupate huduma bora na mzuri”,
Ofisa mipango wa Halmashauri ya Mji Newala, Sofia Makungu wakati akitoa taarifa kuhushu mradi huo amesema, mradi huo ulianza Novemba 2021 wenye lengo la kuwezesha watumishi wa Zahanati hiyo kukaa karibu na eneo lao la kazi.
Hata hivyo kukamilika kwa mradi huo kutachangia kuboresha utoaji wa huduma hizo za afya kwa wananchi wa eneo hilo. Mwenge wa Uhuru umetembelea na kuweka jiwe la msingi miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo ikiwemo sekta ya afya, maji, kikundi cha wajasiliamali barabara, elimu na mingine.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Abdalla Shaib Kaim ameridhia kufungua miradi hiyo ya maendeleo kwani imekidhi vigezo na ubora unaostahili kulingana na thamani ya fedha.