MIRERANI, Arusha: WAZIRI wa Madini, Anthony Mavunde ameshauriwa na wamiliki wa migodi ya madini ya Tanzanite kuwa macho dhidi ya wataalamu waangalizi wa serikali maarufu ’jicho la serikali’.
Imeripotiwa kutoka kwa wamiliki hao kuwa wataalam hao wako kwa ajili ya kujinufaisha na kufanya serikali kupoteza mamilioni ya fedha za kodi katika tathmini ya madini hayo.
Mmoja wa wamiliki wa mgodi wa madini ya Tanzanite ambaye aliomba kuhifadhiwa jina lake amesema pamoja na kupeleka malalamiko kwa Ofisa Madini Mfawidhi Mirerani, Nchahwa Chacha bila majibu wameamua kumwandikia barua Waziri Mvunde juu ya hali hiyo.
Mmiliki huyo amesema waangalizi hao wa serikali mara baada ya mgodi kutoa uzalishaji wa madini ya Tanzanite huja katika mgodi na kuanza kupora madini, kuyaficha na kwenda kwenye tathmni ambapo madini machache na yasiyokuwa na thamani na serikali ndio yanabaki na hivyo kukosa mapato kwani madini mazuri yamechukuliwa na watalaamu hao.
Amesema hali hiyo imekuwa kero kwa wamiliki wa migodi na kufikia hatua kufikisha malalamiko kwa Ofisa Madini Mfawidhi Mirerani lakini hakuna hatua inayochukuliwa na kufikia hatua wamiliki hao kujenga chuki na watalaamu.
Mmiliki mwingine ametoa lawama zote kwa Ofisa Madini Mfawidhi Mirerani, Nchahwa Chacha kwa kuwa kimya bila kuchukua hatua pamoja na kupewa taarifa hiyo na ndio maana wamemwomba Waziri Mavunde afuatilie hilo na ikiwezekana achukue hatua dhidi ya wahujumu wa serikali katika mapato.
‘’Chacha anajua kila kitu na kuna mmoja wa wataalamu hao ni ndugu na kigogo Wizara ya Madini amekuwa na kauli ya jeuri kwa wamiliki wa migodi kwani amekuwa akijinasibu kuwa nyie chongeeni lakini sisi tumekuja kikazi’’alisema mmiliki wa mgodi
Mfanyabiashara mwingine wa Tanzanite Mirerani amesema kuwa Wizara ya Madini kila mtumishi katika sekta hiyo anasharubu ‘kambare’ na wanapoagizwa na serikali kwenda Mirerani kusimamia udhibiti utoroshaji madini na kufanya tathmni sahihi kwa kile kilichopatikana kwa faida ya serikali hiyo inakuwa toufati na kuanza kujitajilisha wao na kuifanya serikali kukosa mapato hatua ambayo wafanyabiashara wanasingiziwa kutorosha madini nje ya nchi kitu ambacho sio kweli.
Akijibu tuhuma hizo kwa njia ya simu ya kiganjani, Ofisa Madini Mfawidhi Mirerani, Nchahwa Chacha amesema hana taarifa rasmi za malalamiko hayo na kusema kuwa Mji wa Mirerani ni mji wa maneno mengi sana na hivyo hawezi kufanyia kazi porojo za mtaani kwani sio utaratibu wa kiserikali.
Chacha amekiri kuwepo kwa wataalamu hao ndani ya ukuta wa migodi ya Tanzanite wenye lengo moja tu la kusimamia uzalishaji na kufanya tathimini sahihi kwenye mgodi unazalishaji madini na sio vinginevyo.
Amesema hayo yanayozungumzwa mtaani yeye kama msimamizi mkuu wa migodi hiyo toka Wizara ya Madini hana taarifa rasmi na kama yapo basi hayajamfikia ofisni kwake na aliwataka wamiliki wa migodi ya Tanzanite kufikisha malalamiko rasmi ofisni kwake ili yaweze kufanyiwa kaquzi na ikibidi hatua stahiki zichukuliwa ikibainika hivyo.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Abdul Mahimbali alipoulizwa suala hilo kwa njia ya simu ya kiganjani amesema kuwa atalifikisha kwa Waziri Mavunde ili aweze kulitolea ufafanuzi zaidi.