Waitara aangua kilio bungeni, asusa

MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ameangua kilio akiwa bungeni na kususia shughuli za bunge kwa kutoka nje, huku akivua koti na tai baada ya kutoridhidhishwa na majibu ya serikali wakati wa kipindi cha maswali na majibu leo Mei 9, 2023.
–
Akiwa ndani ya ukumbi wa bunge, Waitara alitaka kujua lini wananchi wanaodai fidia katika maeneo ya mgodi wa Barrick North Mara Komarera, Nyamichele na Murwambe watalipwa.
Akijibu swali hilo bungeni jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Nishati, Naibu Waziri, Stephen Byabato amesema: “Mgodi wa Barrick North Mara ulionesha nia ya kutaka kuchukua baadhi ya maeneo ya Vijiji vya Komarera, Nyamichele na Murwambie, ambavyo ni sehemu ya vijiji vinavyozunguka mgodi huo.
“Baada ya wananchi wa vijiji hivyo kupata taarifa ya maeneo yao kuhitajiwa na mgodi wa Barrick North Mara, walianza kuongeza majengo harakaharaka (maarufu kama Tegesha), hali hiyo ilipelekea mgodi huo kuachana na maeneo hayo, kwani hayaathiri uendeshaji wa shughuli zao za kila siku,”alijibu Byabato.
Baada ya majibu hayo Waitara hakuridhishwa, hivyo badala ya kuuliza swali la nyongeza kama ulivyo utaratibu alisimama na kuanza kulalamika kutoridhishwa na majibu na kutoka nje ya bunge.